13/2/2015 Wanafunzi wa kike nchini wameaswa kutoogopa kusoma masomo ya sayansi kwani masomo hayo siyo magumu ukilinganisha na mengine wanachotakiwa kufanya ni kuzishika na kuzijua kanuni za somo husika.
Rai hiyo imetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Angaza iliyopo wilayani humo.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema mwanafunzi anayesoma masomo ya sayansi akizishika kanuni anafanya vizuri katika masomo yake tofauti na mwanafunzi wa masomo ya sanaa na kutoa mfano kama mwanafunzi anataka kujua hesabu ni lazima kila siku kabla hajalala afanye mazoezi kwa maswali yasiyopungua 10.
Kwa upande wa uongozi aliwataka wasichana kutoogopa kuomba nafasi mbalimbali za uongozi kwani wakianza uongozi katika umri mdogo watakuwa viongozi wzuri hapo baadaye.
MNEC huyo aliendelea kuwaasa wanafunzi hao na kuwaambia kuwa wao ni ndugu na wakiona mwenzao mvulana au msichana amesimama na mtu wa jinsia tofauti katika mazingira tatanishi wamkanye aache tabia hiyo kwani kilichowapeleka shule ni kusoma na siyo kufanya mapenzi.
“Elimu ni nguzo ya maisha ni lazima mjitambue nyie ni kina nani, mnafanya nini na mnataka kuwa nani hapo baadaye. Someni kwa bidii, waheshimuni na kuwasikiliza walimu wenu kwa kufanya hivyo mtafaulu na kufika chuo kikuu.
“Mkiwa wasomi wazuri mtawezaa kuzitumia fursa zilizopo katika mkoa wetu ikiwa ni pamoja na kuajiriwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya gesi”, alisisitiza Mama Kikwete.
Naye Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi Mzee Alli Mtopa alisema Dunia ya leo ni ya wasomi hivyo basi ni lazima wanafunzi hao wasome ili wafanye kazi katika sekta ya gesi inayopatikana mkoani humo kwani wasiposoma kazi za kitaalamu zitafanywa na watu wengine na wao watabaki kufanya kazi za vibarua na mwisho wake wataandamana kuzuia gesi isitoke.
No comments:
Post a Comment