Thursday, February 19, 2015

TAASISI YA WAMA NA SERIKALI YA JAPANI WATILIANA SAINI MKATABA WA MRADI WA UPANUZI WA SHULE YA SEKONDARI YA WAMA

3
Na Anna Nkinda – Maelezo
 Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na Serikali ya Japani wametiliana saini mkataba wa mradi wa upanuzi wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo Rufiji mkoani Pwani utakaogharimu shilingi milioni mia tisa.
Utiaji saini wa mkataba huo  umefanyika leo katika ofisi za WAMA zilizopo jijini Dar es Salaama kati ya Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Mama Salma Kikwete na Balozi wa Japani nchini Masaki Okada.
Akiongea mara baada ya kusaini makubaliano hayo Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliishukuru Serikali ya Japani kwa kuwajali watanzania na kuwasaidia katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha elimu.
Alisema mradi huo utapanua na kuboresha uwezo wa shule kutoa huduma bora ya elimu ambapo kutakuwa na  upanuzi wa jengo la utawala kwa kuongeza ghorofa moja ili kupata chumba cha walimu ambao wataweza kufanya mikutano yao, kituo cha walimu, na maktaba.
Ujenzi wa chumba maalum cha kompyuta ambacho kitawafanya wanafunzi kusoma somo hilo kwa vitendo, uwekaji wa mitambo ya mawasiliano kwa ajili mtandao wa Internet katika eneo la shule ambao haukuwepo shuleni hapo.
“Pia ninawashukuru kwa msaada wa vitabu vya kiada na ziada ambavyo vitafika hivi karibuni , elimu ni kitabu na ukisoma bila kitabu hutakuwa na mapana zaidi, tukipata vitabu vya ziada vitasaidia kujenga ufahamu wa mtoto kuweza kuchanganua mambo mbalimbali”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Balozi Okada alisema mradi huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni ujenzi wa maabara ya kompyuta pamoja na kutoa vifaa muhimu na kuunganisha Broadband Internet kwenye maabara.
Balozi Okada alisema, “Baada ya mradi huu kukamilika sio tu wanafunzi wataweza kujifunza kompyuta bali pia watatumia internet kupata taarifa nyingi na za kisasa zinazopatikana mtandaoni.
“Sehemu ya  pili ni upanuzi wa jengo la utawala. Mradi huu ukikamilika wanafunzi hawatapata tabu ya kutafuta walimu kwa ajili ya kuuliza maswali kuhusu masomo. Ninaamini kwamba mazingira bora kwa walimu yanaboresha mazingira ya kusomea kwa wanafunzi”.
Aidha Balozi Okada alisema Hayao  Nakayama ambaye ni mtu wa kwanza kutoa ufadhili kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ametoa zaidi ya milioni mia moja na themanini ambazo zitatumika kwa ajili ya  kununulia gari la dharura la kubebea wagonjwa na maelfu ya vitabu ambavyo vitasafirishwa siku za karibuni kutoka nchini Japani.
Balozi huyo alisema vitabu hivyo siyo tu vya masomo ya sayansi na hisabati vinavyohitajika kuongeza ujuzi  lakini pia kuna vitabu vya kiingereza na kiswahili kama vile hadithi, riwaya halisi pamoja na wasifu wa watu mashuhuri wanaume na wanawake kutoka duniani kote ikiwamo Japani.
“Wanafunzi watajifunza hadithi za mashujaa waliopigania elimu kwa wanawake na waasisi wa kampuni kubwa kama vile Panasonic na Honda. Wataweza kupata watu wa mfano wa kuigwa kati ya hao wataweza kujifunza kutokana na  maisha yao jinsi walivyotekeleza ndoto zao na kuishi siyo tu kwa ajili yao binafsi bali kwa familia, marafiki na watu katika jamii na taifa kwa ujumla”, Balozi Okada alisema.
Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama yenye wanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza hadi cha tano  wengi wao wakiwa ni watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ilianza mwaka 2010 ikiwa na wanafunzi 83 na hadi sasa ina wanafunzi 366.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...