Sunday, February 22, 2015

MAMA SALMA KIKWETE MGENI RASMI KWENYE SHEREHE YA MAULID YA KUZALIWA MTUME MUHAMMAD (S.A.W) HUKO WETE-PEMBA

mam1
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Karume huko Pemba na kupokewa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Ndugu Mwanajuma Majid Abdalla tarehe 20.2.2015. Mama Salma alialikwa Pemba kama Mgeni Rasmi kwenye sherehe ya Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) iliyoandaliwa na Al-Madrasat Jabal- Hiraa.PICHA NA JOHN  LUKUWI 
  mam2
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na viongozi mbalimbali waliofika kumpokea wakati alipowasili kwenye Uwanja wa ndege wa Karume huko Pemba kwa ziara ya kikazi ya siku moja kisiwani humo tarehe 20.2.2015.mam3
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipokewa rasmi kwa kuvishwa shada na wasichana wa Almadrsat Jabal-Hiraa mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Shule ya Utaani huko Wete Pemba ilikofanyika sherehe ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambapo Mama Salma Kikwete alikuwa mgeni rasmi tarehe 20.2.2015.mam4
Mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) kwenye Shule ya Utaani huko Wete Pemba wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi Mama Salma Kikwete (hayupo pichani) aliyokuwa akitoa wa viongozi na wananchi waliohudhuria sherehe hizo tarehe 20.2.2015.
mam5mam6
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akitoa nasaha zake kwenye Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) iliyofanyika kwenye Shule ya Utaani huko Wete katika Mkoa wa Kaskazini Pemba huku mamia ya watu wakimsikiliza. Mama Salma alikuwa Mgeni rasmi kwenye sherehe hiyo iliyofanyika tarehe 20.2.2015.
mam7………………………………………………………….
Na Anna Nkinda – Pemba
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wanawake wa  mkoa wa Kaskazini Pemba kuhakikisha watoto wao wanasoma kwa bidii hadi  elimu ya juu kwa kufanya hivyo wataweza kuzitumia fursa zilizopo na kushika nafasi mbalimbali za uongozi na hivyo kufika ngazi ya maamuzi.
Mama Kikwete alitoa rai hiyo jana wakati wa sherehe za Maulid ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) zilizoandaliwa na  wanawake wa madrasa ya  Jabal – Hiraa na  kufanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Utaani Kaskazini Pemba.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema Mtume Muhammad S.A.W. alisimamia umuhimu wa elimu kwa kuona kuwa ili kuweza kuishi na kustawi katika dunia hakuna  budi kupata elimu zote ya ahera na ya duniani ambayo itawezesha kufungua milango ya fursa za duniani na za akhera.
“Sisi waislamu tumekuwa tukilalamika kuachwa nyuma kimaendeleo na wenzetu. Sababu kubwa ni kutotia mkazo kwenye elimu na hata pale tunapowasomesha watoto wetu skuli basi tunapuuzia ile ya watoto wa kike. Hili bahati mbaya liko kwetu sisi waislamu wa Afrika”.
Mimi nimebahatika kutembea duniani, nimeona wanawake wa kiislamu, tena kutoka nchi za kiislamu wakifanya mambo makubwa, wana vyeo na daraja kubwa kutokana na elimu na ustadi wao. Hawajaacha kuswali, hawajaacha kuolewa, wala kuacha kuwa wake wa kiislamu”, alisema Mama Kikwete.
Alitoa mfano wa nchi ya   Misri ambapo asilimia 49 ya wanafunzi wa vyuo vikuu ni wanawake na ni waislamu. Iran asilimia 60 ya wanafunzi wa vyuo vikuu ni wanawake.
Alisema wasiposomesha watoto wao haswa watoto wa kike wataendelea kujitumbukiza katika umasikini na hatimaye kuchuma dhambi kwa kuwaonea husda waliofanikiwa. Mtoto wa mama wa kiislamu aliyesoma,  naye ana nafasi kubwa ya  kuwa na mafanikio katika maisha.
Kwa upande wa malezi aliwasihi wanawake  hao kuwa chanzo cha mabadiliko kwani wao ndiyo walezi wa watoto na Taifa, wawalee watoto  katika unyenyekevu, kwa imani na kuhakikisha wanavaa mavazi ya heshima yanayokubalika katika jamii yao.
Mama Kikwete pia aliwahimiza wanawake hao kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu kwakuwa maisha ya binadamu yanasiasa ndani yake na siasa huleta maendeleo. Kwa wale watakaojitokeza wawaunge mkono na kuchagua amani, usalama na maendeleo.
Alihimiza, “Jitokezeni kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura zoezi la kujiandikisha litaanza wakati wowote. Safari hii vitatumika vitambulisho vipya vya kisasa. Wasiojiandikisha na kupata vitambulisho hivi hawataweza kupiga Kura ya Maoni ya Katiba inayopendekezwa wala kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu”.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mwanajuma Majid Abdalla alimshukuru Mama Kikwete kwa kukubali kwake kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo na kumuomba Mwenyezi Mungu amzidishie kheri katika maisha yake.
Aliwasisitiza kina mama waliohudhuria sherehe hizo kutenga muda wao kwa ajili ya kwenda madrasa kupata elimu ya ahera  na pia wajifunze elimu ya dunia ambazo zitawasaidia  katika maisha yao .
“Katika suala la elimu wanawake tuko nyuma kwa madai kuwa tunashughuli nyingi za kifamilia na hivyo kukosa muda wa kujifunza, nawaomba tengeni muda wenu mkajifunze kwani kutokuwa na elimu ya dini na dunia  kutakufanya siku moja  ukashindwa kufanya mambo ya maana pale  utakapokutwa na tatizo ukiwa peke yako”, alisema Mwanajuma.
Akisoma risala ya madrasa Jabal – Hiraa Khadija Suleiman Muhammed alisema ilianza na wanawake watatu na mwanaumme mmoja ambaye ni Mwenyekiti hadi sasa ina wanafunzi 104  kati ya hao wanawake 63 na wanaume 41.
Khadija alisema  walimu wa madrasa hiyo wanafundisha kwa njia ya kujitolea  hujipatia kipato kwa kualikwa katika shughuli za Maulid na katika shughuli hizo hutumia mashine za kukodi lakini kama watakuwa na mashine zao zitawasaidia kutatua matatizo waliyo nayo.
 Alizitaja mashine hizo kuwa ni boxi mbili za spika, pawa yenye warts 2000, wireless mic mbili na mixer thamani yake ikiwa ni shilingi milioni tatu na laki moja.
“Tunawakumbusha viongozi wa dini tutumie nafasi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kuielimisha jamii kuacha kuuza au kutumia madawa ya kulevya na kujilinda na ugonjwa wa Ukimwi kwasababu ndiyo janga kubwa kwa taifa letu”, alisema Khadija.
Aliyataja mafanikio waliyoyapata kuwa ni wakati madrasa hiyo inaanza walikuwa wanatumia  jengo la mtu lakini hivi sasa wamefanikiwa kupata kiwanja na kujenga jengo la vyumba vinne ambalo halijakamilika lenye  madarasa ya kusomea mawili, chumba cha wageni kimoja, ofisi moja na vyoo viwili.
Mama Kikwete aliipatia madrasa hiyo mifuko 25 ya saruji ambayo waliihitaji kwa ajili ya kumalizia ujenzi,  vitabu vya kusomeshea vya Mas-hafu na juzuu. Pia aliahidi kuziunga mkono madrasa nyingine sita zilizohudhuria sherehe hiyo.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...