Saturday, November 01, 2014

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi afungua rasmi Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)


 
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu, akimsindikiza Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Japan Kidata kuelekea kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga, katika Ufunguzi Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu, akimsindikiza Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Japan Kidata kuelekea kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga, katika Ufunguzi Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo.

Katibu wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa, Mecktilda Mihayo akijadiliana jambo na Veronica Mtemi na Katibu Msaidizi wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa, Adolph Kasegenya wakati wakisubiri kumpokea Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Japan Kidata wakisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni Chiku Gallawa kabla ya kuelekea kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga, katika Ufunguzi Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo.
Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Japan Kidata akikaribishwa na Katibu wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa, Mecktilda Mihayo kuelekea kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga, katika Ufunguzi Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo.
Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Japan Kidata akikaribishwa na Mkurugenzi wa Usimamizi Miliki wa NHC, Hamad Abdallah huku Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma kwa Jamii (Katikati), Susan Omari kuelekea kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga, katika Ufunguzi Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu akimuongoza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo JapanKidata kuingia kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga, katika Ufunguzi Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa NHC, Martin Mdoe akijadiliana jambo na Meneja Madeni wa Shirika la Nyumba la Taifa, Joseph Mwanasenga wakati wakisubiri Mgeni rasmi.
 Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakiimba wimbo wa 'Solidarity Forever' ikiwa ni ishara ya kuhimiza ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi wakati Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Japan Kidata walipokuwa wakiingia kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga, katika Ufunguzi Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo.
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Japan Kidata wakiwa wamewasili kwenye meza yao.
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu akiwahutubia wajumbe wa Kikao Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Sehemu ya Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakifuatilia Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo kinachofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga,
 Meneja wa Manunuzi wa NHC, Michael Chilongani, Afisa Mauzo wa NHC Gibson Mwaigomole wakifuatilia Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo kinachofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga,
Meneja wa Huduma kwa Jamii, Muungano Saguya na Pastory Pauline wakifuatilia Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo kinachofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga,
Meneja wa Huduma kwa Jamii, Muungano Saguya na Emmanuel Abdallah wakifuatilia Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo kinachofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga,
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Ilala, Jackson Maagi na Meneja wa NHC Shinyanga, Ramadhani Macha wakifuatilia Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo kinachofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga,
Meneja Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu, Bulla Boma na Afisa kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakifuatilia Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo kinachofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Tanga Beach Resort Tanga,

Picha ya pamoja ya Wajumbe wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa kinachofanyika leo hoteli ya Tanga Beacha Resort, Tanga.

Picha ya pamoja ya Wajumbe wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa kinachofanyika leo hoteli ya Tanga Beacha Resort, Tanga.

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&7
Shirika la Nyumba la Taifa 

HOTUBA YA GENI RASMI, KATIBU MKUU, WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI, BW. ALFAYO JAPAN KIDATA, KWENYE UFUNGUZI WA KIKAO CHA BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI, JIJINI TANGA TAREHE 1 NOVEMBA, 2014

Ndugu Nehemia Kyando Mchechu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi,
Ndugu Wakurugenzi,
Ndugu Wajumbe wa Baraza,
Wageni Waalikwa,
Wanahabari,
Mabibi na Mabwana,

Awali ya yote, napenda nianze kwa kuishukuru Menejimenti ya Shirika, kwa kunipa heshima ya kuja kuwa Mgeni Rasmi kwenye ufunguzi wa Baraza hili. Nawashukuru sana.

Nawashukuru kwa sababu tukio hili la leo limenipa fursa ya kukutana na watendaji wakuu na wawakilishi wa wafanyakazi kutoka Mikoa yote ya Shirika kwa mara ya kwanza tangu niteuliwe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara yetu. Hivyo, ni fursa kwangu kuweza kufikisha ujumbe kwa wafanyakazi na umma juu ya Shirika letu.

Ndugu Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kuwapa wajumbe wote pole kwa safari ya masafa marefu mpaka kufika hapa Tanga. Naamini kuwa uchovu wenu umemalizwa na hali nzuri ya hewa ya Jiji hili la Tanga pamoja na ukarimu wa Wana-Tanga ukiambatana na usemi wao “waja leo, warudi leo”. Bila shaka hamtarudi leo kama usemi huu unavyosema maana Tanga kuna vivutio vingi vya kufurahia ikiwemo bandari kongwe, mapango ya Amboni na fukwe zenye mandhari nzuri. Msije mkaondoka Tanga bila kula ugali wa mhogo maarufu kama BADA, kuku wa mchemsho na mchunga.

Ndugu Mwenyekiti, nimefahamishwa kuwa Baraza hili limetanguliwa na mikutano ya Mameneja wa Mikoa na mapitio ya Mpango Mkakati wenu kwa nia ya kutengeneza Mpango Mkakati  mwingine kwa miaka kumi ijayo. Sisi katika Wizara tumefarijika sana kuona kuwa Menejimenti ya Shirika inatambua umuhimu wa kuwapatia viongozi wake wa Mikoa ujuzi katika uongozi kwani uongozi bora na makini huchangia sana katika kuleta tija. Aidha, niwapongeze kwa kutengeneza Mpango Mkakati mzuri wa miaka mitano ambao unamalizika mwaka ujao. Kila mmoja na hata Taifa letu linatambua kuwa Mpango Mkakati wenu umeleta tija kubwa na mmeweza kuutekeleza kwa mafanikio makubwa sana. Hongereni sana.
Ndugu Mwenyekiti, nimeelezwa pia kuwa ajenda za kikao cha Baraza hili zitahusu kujadili mambo ya utendaji kwa ujumla yanayohusu maendeleo ya Shirika mliyojiwekea kwenye Mpango Mkakati wa miaka mitano. Aidha, nimeelezwa kuwa kikao chenu kitapitia mizania ya hesabu za Shirika kwa mwaka 2014/2015, pamoja na kujadili taarifa za utekelezaji wa mambo mliyojiwekea katika Mpango Mkakati wenu. Naupongeza sana utaratibu huu maana unaleta mezani kwa pamoja utekelezaji wa majukumu ya kazi na kuainisha changamoto zilizokuwepo kwa nia ya kuzipatia ufumbuzi uliyo makini zaidi.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, sina haja ya kusisitiza umuhimu wa ajenda zote hizi zilizoko mbele yenu, kwani naamini wajumbe wote wa Baraza hili mnatambua umuhimu wake. Hivyo, ni matarajio yangu kuwa ajenda hizi, ambazo zinagusa uhai na maendeleo ya Shirika letu, mtazijadili kwa kina ili hatimaye muweze kutoka na maazimio makini yatakayoliwezesha Shirika hili kuongeza tija na kukidhi matarajiyo ya umma wa watanzania, ambayo kwa sasa yako juu sana kutokana na imani mliyowajengea.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, napenda pia kuchukua fursa hii kuwapongeza wafanyakazi wa Shirika kwa kutenda kazi zenu kwa ufanisi mkubwa. Inafurahisha kuona kuwa hivi sasa mmejipanga vilivyo kupanua shughuli za ujenzi wa nyumba hususan za gharama nafuu katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Kipekee niwapongeze kwa kurejesha utaratibu aliouanzisha Baba wa Taifa wa kuanza kwa kasi ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika miji mbalimbali ya Halmashauri za Miji na Wilaya nchini. Nafahamu kuwa hivi sasa mmeshaifikia mikoa 19 na mnayo matumaini makubwa ya kufikia mikoa yote kufikia Desemba mwaka huu. Utaratibu huu unaolenga kuwawezesha wananchi wa kipato cha kati na chini kumiliki nyumba, umepongezwa sana na Serikali Kuu na viongozi mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. Hivyo, mnayo dhima na jukumu kubwa la kuusimamia mpango huu ili ndoto hiyo ya kuwawezesha watu wengi kumiliki nyumba iweze kutimizwa. Bila shaka mkifikia lengo hilo, mtakuwa mmeweka msingi mkubwa wa kukumbukwa katika Taifa letu na vizazi vijavyo kama tunavyomkumbuka Baba wa Taifa wa kueneza ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika miji mingi baada ya Uhuru wa Taifa letu.
Ili kuzifanya nyumba hizi mnazojenga kuwa nafuu, narudia kusisitiza agizo alilolitoa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Halmashauri za Miji na Wilaya zilipatie Shirika la Nyumba na waendelezaji wengine wa Miliki maeneo ya kujenga nyumba hizo bila kuhitaji fidia kubwa. Aidha, Wizara yangu itaendelea kuzishawishi taasisi zinazotoa huduma za msingi za makazi kama vile umeme, maji na barabara kutimiza wajibu wao kwa kupeleka huduma hizo katika maeneo ya ujenzi wa nyumba. Kwa kuwa hili pia ni agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu alilolitoa wakati akizindua ujenzi wa nyumba za NHC, Medeli, Dodoma tarehe 13/8/2011. Nina imani kuwa taasisi zote husika zitatekeleza jambo hili. Napenda kulipongeza Shirika la umeme Tanzania kwa kuanza kupeleka huduma zake katika maeneo mapya ya ujenzi wa nyumba. Niwahakikishie kuwa Wizara yangu itaendelea kufuatilia kwa karibu jambo hili.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, nafarijika pia kuwapongeza kwa dhati kwa kuboresha huduma zenu mnazowapa watanzania. Hivi sasa unapopita katika miji mingi hapa nchini unashuhudia nyumba nyingi za Shirika zikipendeza baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa. Vilevile, kipekee niwapongeze kwa kuweza kukusanya kodi na malimbikizo yaliyokuwepo huko nyuma bila woga jambo ambalo limewezesha kujenga nidhamu kwa wapangaji wenu ya kulipa kodi. Hivi sasa Wizara yangu haipokei malalamiko mengi kutoka kwa wapangaji na wafanyakazi wenu kutokana na Menejimenti kujitahidi kuondoa kero mbalimbali kwa kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi anatenda kazi zake kwa uwazi, uadilifu na weledi wa hali ya juu. Mambo hayo yote kwa ujumla yamewaongezea heshima kubwa na kujenga taswira nzuri ya Shirika katika jamii ya watanzania. Hongereni sana na endeleeni kutenda kazi zenu kwa juhudi na maarifa mkitambua umuhimu mkubwa wa sekta ya nyumba tuliyowapa dhamana ya kuisimamia.
Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, nichukue pia fursa hii kuwapongeza kwa dhati kwa uamuzi wenu wa kizalendo mlioufanya na kuutekeleza wa kuwapatia vijana mashine za kufyatulia matofali katika Halmashauri zote za Wilaya Tanzania. Uamuzi huu makini na ulioutukuka umesaidia juhudi za serikali za kuondoa umaskini miongoni mwa vijana kwa kuwapatia ajira vijana hao. Kama mnavyofahamu vijana wasipokuwa na kazi ya kufanya hujiingiza katika uhalifu na kuhatarisha amani ya nchi. Tumefurahi kuona kuwa hivi sasa mmeshirikiana na Mamlaka ya Ufundi Stadi nchini (VETA) kuwpa vijana mafunzo ya namna ya kutumia mashine hizo kutengenezea matofali. Teknolojia hii mliyoibuni ya kutengeneza matofali kwa kutumia mashine hizi inatumia sementi kidogo kuzalisha matofali na kwa hiyo  haiharibu mazingira kwa kuwa hakuna miti inayokatwa ili kuchomea matofali. Tunaupongeza utaratibu huu ambao umetoa ajira kwa vijana na tunataraji kuwa mtaongeza ushirikiano huo na VETA kwenye maeneo mengine ya ujenzi kama upigaji wa rangi, useremala, umeme, uwekaji marumaru na bomba ili kuwapa vijana wengi zaidi ujuzi na ajira. Endeleeni na utaratibu huu ambao hata Rais wetu Mheshimiwa Dk. Jakaya Kikwete ameupongeza sana wakati akihutubia Taifa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kitaifa yalifanyika Jijini Mbeya. Hivyo,nichukue fursa hii kuwasihi Mameneja wa Shirika wa Mikoa kusimamia utekelezaji wa program hii ili iweze kuleta tija iliyokusudiwa na Shirika na Serikali yetu.
Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, kama mnavyofahamu hapa nchini kuna uhaba mkubwa wa nyumba unaokadiriwa kufikia nyumba milioni tatu. Pamoja na juhudi na ubunifu mbalimbali mliyoufanya uliosaidia kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba za kada zote, Serikali yenu inaamini kuwa mkiongeza kasi zaidi katika ujenzi wa nyumba, licha ya kuwa mtakuwa mmetekeleza ilani ya uchaguzi ya chama tawala, mtakuwa pia mmeisaidia Serikali katika juhudi zake za kuondoa umaskini nchini.
Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, nawaomba muendelee na juhudi hizo mlizozionyesha ili hatimaye chombo hiki muhimu cha serikali kiweze kukidhi matarajio ya umma wa Watanzania.  Kama mlivyokwishasikia, upande wa serikali tunajitahidi kuboresha sera ya nyumba na sheria mbalimbali ili kufanya sekta ya nyumba hapa nchini iweze kuchangia kikamilifu pato la Taifa.
Ndugu Mwenyekiti na Ndugu wajumbe, Serikali inafahamu kuwa zipo changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya nyumba ikiwemo gharama kubwa  ya vifaa vya ujenzi na upatikanaji wa mikopo ya nyumba ya muda mrefu yenye riba nafuu.  Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inazifanyia kazi changamoto hizo ili kuifanya sekta ya nyumba iwe na mchango mkubwa wa uchumi na jamii kwa ujumla. Hata hivyo, nyie kama wataalamu wa ujenzi, mnapaswa mara kwa mara, na hata kupitia kikao muhimu kama hiki, kuishauri serikali yenu namna bora ya kuwezesha wananchi kujengewa au kujenga nyumba za gharama nafuu, kama mkakati mmojawapo wa kuondoa umaskini kwa wananchi wetu.
Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, naelewa kuwa kodi ya nyumba kwa muda mrefu sasa imekuwa ndiyo uti wa mgongo wa mapato ya Shirika. Pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuikusanya kodi hiyo, napenda vile vile nitoe wito kwa wapangaji wote nchini wanaodaiwa kodi na malimbikizo wajitahidi kulipa kodi hiyo ili Shirika liweze kujenga nyumba mpya na kutengeneza nyumba zilizopo kama ilivyopangwa. Wajibu huo wa kulipa kodi umo ndani ya mikataba yao ya upangaji. Wapangaji wafahamu kuwa kodi ndiyo inayotumika kutoa huduma bora kwao na kwa wananchi wengine. Wafahamu kuwa nyumba wanazopanga kimsingi ni mali ya watanzania wote na kwamba wao wamebahatika tu kupata fursa hiyo adimu ambayo kimsingi wanapaswa kuienzi kwa kulipa kodi kwa wakati. Aidha, wafahamu kuwa kodi ya nyumba za Shirika iko chini ukilinganisha na wamiliki wengine wa nyumba nchini. Ni vema sasa Shirika likarekebisha viwango vya kodi ya nyumba zenu ili viendane na hali halisi ya sasa, inagawa haitafikia viwango vinavyotozwa na wamiliki wengine.
Ndugu Mwenyekiti na Ndugu wajumbe, yapo mengi ya kuongea. Hata hivyo, nisingependa kuwachosha kabla ya kuanza kazi kubwa inayowasubiri. Hivyo, naomba niishie hapa kwa kuwashukuru tena kwa kunipa heshima ya kuzungumza nanyi kupitia Baraza hili. Ni matumaini yangu kuwa maazimio mtakayopitisha hapa mtakwenda kuyatekeleza kwa vitendo na kwa uadilifu mkubwa, ili kuliwezesha Shirika letu kutoa huduma za makazi zilizo bora kwa wananchi.

Baada ya kusema hayo, Ndugu Mwenyekiti, sasa napenda kutamka kuwa Kikao cha Baraza lenu la Wafanyakazi kimefunguliwa rasmi. Nawatakia kikao chema na ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...