Tuesday, November 04, 2014

JESHI LA POLISI KANDA MAALUM YA DAR LAWAACHIA HURU MWENYEKITI WA BODI YA TPDC NA KAIMU MKURUGENZI MKUU

TPDC (1)
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewaachia huru Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (Tanzania Petroleum Development Corporation – TPDC) Mh. MICHAEL PETRO MWANDA na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo JAMES ANDILILE kusubiri  ufafanuzi wa Bunge kutokana na tuhuma zinazowakabili. Awali, jana tarehe 03/10/2014 saa tano asubuhi katika ukumbi wa Bunge uliopo jijini Dar es Salaam katika chumba cha mikutano kulikuwa na kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mwenyekiti akiwa ni Mh. ZITTO ZUBERY KABWE (MB) na makamu wake ni Mh. DEO FILIKUNJOMBE (MB).
Katika kikao hicho agenda ya mkutano ilikuwa ni kuwasilisha mahesabu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi kinachoishia tarehe 30 June, 2013. Baada ya majadiliano ya muda kuhusu hati mbalimbali zilizotakiwa na Kamati hiyo ya Bunge hatimaye Mwenyekiti wa Kamati Mh.  Zitto Zubery Kabwe alitoa maagizo kwa askari wa Polisi waliokuwepo katika eneo hilo kwa masuala ya ulinzi kuwa Mwenyekiti wa bodi ya TPDC na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wafikishwe kituo cha polisi Kati.
Kutokana na maelezo ya mashahidi waliokuwepo kwenye tukio hilo katika ukumbi wa Bunge Mwenyekiti Zitto alisema wapelekwe Polisi waende kusubiri mwongozo wa Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye atawasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa maagizo ya mwisho. Mara baada ya agizo hilo watu hao walifikishwa kituo cha Polisi Kati chini ya ulinzi. 
Uongozi wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ulishindwa kuchukua hatua zaidi ya hapo kwani shauri hilo halikuwa na mlalamikaji aliyekuja kufungua jalada na kutoa ufafanuzi kuhusu mashtaka yanayowakabili viongozi wa TPDC. Aidha, maafisa wawili wa secretarieti ya Bunge waliitwa Polisi kutoa ufafanuzi kuhusu kadhia hii wakiwepo pia mawakili wa watuhumiwa na hatimaye kilifanyika kikao cha dharura ili kupata ufafanuzi wa kisheria.
Hatimaye iligundulika kwamba katika sheria ya HAKI, KINGA na MADARAKA ya Bunge sura ya 296 Kif 12 (3) kinaonyesha kwamba mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali alitakiwa kwanza apendekeze kwa Mhe. Spika wa Bunge juu ya jambo lolote aliloliona kama ni kosa. 
Mhe. Spika akisharidhika kuhusu tuhuma zozote zilizoletwa mezani kwake na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, ndipo anamwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili suala hilo lipate ufafanuzi wa kisheria ikiwa ni pamoja na hatua za kisheria zinazostahili kuchukuliwa. 
Katika kikao hicho na jopo la wanasheria iligundulika kwamba katika sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya bunge, agizo la kukamatwa watu hao lililotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge  lilihita kuzingatiwa kwa taratibu tajwa hapo juu kwanza kabla ya utekelezaji wake. 
Hatimaye ilionekana hakuna sababu ya kuendelea kuwashikilia viongozi hao na badala yake wameachiwa huru tukisubiri taratibu na sheria kama ilivyoelezwa hapo juu.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...