Monday, September 01, 2014

TUME YA UTUMISHI WA UMMA YAENDELEA KUIMARISHA UZINGATIAJI WA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU ZA MASUALA YA AJIRA


Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma Bi. Neema Tawale akieleza kwa waandishi wa Habari (Hawapo pichani) kuhusu tathmini ya Tume juu ya uzingatiaji wa sheria,kanuni na taratibu za masuala ya ajira katika utumishi wa uuma, wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Katibu Msaidizi wa Tume hiyo Bw. John Mbisso.

Kaimu Katibu Msaidizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma Bw. John Mbisso  akiongea na waandishi wa (Hawapo pichani) kuhusu jitihada wanazozifanya katika kuwaongezea uelewa wadau juu ya haki na wajibu wao katika masuala ya ajira katika utumishi wa umma, wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Kulia ni Naibu Katibu wa Tume hiyo Bi. Neema Tawale.


Baadhi ya waandishi wa habari waliwasikiliza wawasilishaji toka Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
(Picha na Hassan Silayo)
Na Fatma Salum
Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma imeendelea kuimarisha Kiwango cha uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma  Bi Neema Tawale katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Bi Tawale alisema kuwa tathmini kuhusu uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za  masuala ya ajira iliyofanywa na Tume hiyo mwaka 2010/2011 katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekretarieti za Mikoa imebainisha kuwa kiwango cha uzingatiaji kimeongezeka hadi kufikia asilimia 64 kwenye vipengele  vya Uajiri, Upimaji wa Utendaji Kazi wa Wazi (OPRAS), Likizo ya Mwaka na Likizo ya Ugonjwa.
Akifafanua zaidi Bi Tawale aliongeza kuwa ukilinganisha na utafiti wa kwanza uliofanyika mwaka 2005/2006 ambapo kiwango kilikuwa ni asilimia 50 ongezeko hilo limetokana na elimu inayotolewa na Tume kwa wadau kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya mwaka 2002 na Marekebisho yake Na.18 ya mwaka 2007.
“Tume ya Utumishi wa Umma inajitahidi kuweka mikakati ili kuhakikisha inakabiliana na changamoto za masuala ya ajira katika kuongeza uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu kwa kuendelea kutoa elimu kupitia miongozo, vipindi kwenye vyombo vya habari na maonyesho mbalimbali ya kitaifa”. Alisema Bi Tawale.
Aidha Bi Tawale alisema kuwa Mwongozo uliotolewa na Tume hiyo kuhusu masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma unawawezesha Waajiri na Mamlaka za Ajira kufuata taratibu wanaposhughulikia masuala ya ajira kwenye mamlaka zao.
Aliongeza kuwa katika kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za ajira zinatekelezwa ipasavyo Tume huagiza Waajiri au Mamlaka za Ajira kuchukuliwa hatua ikiwemo kuwaita mbele ya Tume kujieleza ikithibitika wamekiuka sheria au wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
Naye Kaimu Katibu Msaidizi wa Tume hiyo Bw. John Mbisso alitoa msisitizo kwa waajiri kushughulikia masuala ya ajira ya watumishi wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuepuka migogoro na kupunguza malalamiko kuhusu masuala ya ajira kwenye utumishi wa umma.

No comments:

Rais Samia Awasili Dar es Salaam kwa Treni ya Umeme ya SGR Akitokea Dodoma

Dar es Salaam, 22 Januari 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili jijini Dar es Salaa...