Imeelezwa kuwa, utaratibu wa kisheria unaowataka wafanyabiashara wa dhahabu nchini kuuza angalau asilimia 20 ya dhahabu wanayozalisha kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni hatua muhimu ya kulinda uchumi wa taifa sambamba na kuimarisha thamani ya shilingi.
Hayo yameelezwa leo Septemba 27, 2025 na Mjiolojia Mwandamizi kutoka Wizara ya Madini, Benjamin Mikomangwa, wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) katika Maonesho ya 8 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita.
Amesema ununuzi wa dhahabu kupitia BoT unalenga kukabiliana na changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni na kuongeza akiba ya taifa kupitia dhahabu inayohifadhiwa kwenye hazina ya benki hiyo.
"Ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu una faida nyingi, ikiwemo kuongeza imani ya wawekezaji, kulinda thamani ya shilingi na kuimarisha uthabiti wa uchumi hata katika nyakati za misukosuko ya kifedha duniani,” amesema Mikomangwa.
Ametaja faida nyingine kuwa ni pamoja na kinga dhidi ya mfumuko wa bei kwa kuwa thamani ya dhahabu huongezeka pindi sarafu za kawaida zinapopungua thamani, hivyo kusaidia kulinda uwezo wa ununuzi wa wananchi pamoja na Nguvu ya ushawishi kimataifa kwani akiba kubwa ya dhahabu huongeza heshima ya nchi kwenye majukwaa ya kifedha duniani na kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya masharti nafuu.
Ameongeza kuwa akiba hiyo husaidia kujenga imani kwa soko la ndani na nje kwa kuwa akiba thabiti ya dhahabu huimarisha uthabiti wa mfumo wa kifedha, jambo linalovutia wawekezaji wa kigeni na kulinda rasilimali za ndani.
Mikomangwa amesisitiza kuwa uwepo wa akiba ya dhahabu husaidia kuhakikishia nchi wakati wa dharura kwani katika nyakati za migogoro ya kifedha au kuporomoka kwa masoko, akiba ya hiyo hutumika kama msaada wa haraka wa kifedha kwa Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa za kifedha za Benki Kuu ya Tanzania za Agosti 2025, zinaonesha Benki hiyo imeimarisha akiba yake ya dhahabu kufikia tani 9 dhahabu zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 2 kufikia Agosti 31, 2025.
No comments:
Post a Comment