New York, Marekani – Septemba 25, 2025
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hasara na Maafa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi (Loss and Damage Fund), Bw. Ibrahima Diong. Mazungumzo hayo yalifanyika pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea Jijini New York, Marekani.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wawili walijadili masuala muhimu yanayohusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwa mataifa ya Afrika, ikiwemo Tanzania. Aidha, waligusia changamoto ya ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya mfuko huo, ili kuziwezesha nchi zinazoendelea kuchukua hatua za kukabiliana na madhara makubwa yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi licha ya uhaba wa rasilimali.
Mfuko wa Hasara na Maafa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni mpango wa kifedha ulioundwa mahsusi kusaidia nchi zinazoendelea ambazo zimeathiriwa zaidi na majanga kama mafuriko, ukame, na kupanda kwa kina cha bahari. Lengo lake kuu ni kufidia hasara zisizoepukika pamoja na kusaidia kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa, kuhamisha jamii zilizo hatarini, na kurejesha ardhi ya kilimo na maeneo ya pwani.
Aidha, mfuko huu unalenga kusaidia zaidi mataifa yaliyo hatarini, hususan nchi ndogo za visiwa na zile zenye kipato cha chini, ambazo kimsingi zimechangia kwa kiwango kidogo sana katika uzalishaji wa gesi chafu duniani.
Mfuko wa Hasara na Maafa ulianzishwa rasmi mwaka 2022 katika Mkutano wa 27 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) uliofanyika Sharm El-Sheikh, Misri, baada ya miongo kadhaa ya mjadala. Wakati wa Mkutano wa COP28 huko Dubai, nchi wanachama zilikubaliana kuanza utekelezaji wake rasmi.
Mazungumzo kati ya Makamu wa Rais Dkt. Mpango na Bw. Diong yameonesha dhamira ya Tanzania kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mfuko huu, ili kuhakikisha wananchi wanalindwa dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya Taifa yanaendelea bila kuyumba.
No comments:
Post a Comment