Na Mwandishi Wetu, Handeni
MKUU wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amekagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilayani humo na kutoa maagizo ya maboresho mbalimbali ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa viwango vinavyotarajiwa.
Mradi huu unaotarajiwa kugharimu Shilingi Bilioni 1.6, unajumuisha ujenzi wa majengo tisa, na Mhe. Nyamwese amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha bweni la wanafunzi linaingizwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji, ili wanafunzi waweze kuanza kupata mafunzo mara tu awamu hiyo itakapokamilika.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa mradi, Mhe. Nyamwese amewataka mshauri elekezi na msimamizi wa mradi kushirikiana kwa karibu ili mpango huo wa kuingiza bweni katika awamu ya kwanza ushambuliwe bila kuchelewa.
Aidha, ameelekeza Jeshi la Zimamoto lishirikishwe mapema ili kutoa ushauri kuhusu vifaa vya usalama vinavyohitajika kabla ya kukamilika kwa mradi.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya amewapongeza wasimamizi wa mradi kwa kazi nzuri iliyofanywa hadi sasa, huku akisisitiza kwamba mapungufu yaliyojitokeza yashughulikiwe mara moja ili mradi usikose kufikia malengo yake kwa wakati.
No comments:
Post a Comment