Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Thabit Kombo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar Kazi na Uwekezaji Mhe. Shariff Ali Shariff katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Mabalozi wa Tanzania mara baada ya kuhutubia Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Thabit Kombo wakati akiondoka katika Jengo la Makao
Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani mara baada ya
kuhutubia Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika
Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inalaani kuibuka upya kwa ukiukwaji wa sheria za kimataifa na kupelekea matumizi ya nguvu kama njia ya kutatua migogoro hali inayopelekea ukatili uliokithiri kwa binadamu hususani watoto, wanawake, wazee pamoja na wagonjwa katika maeneo ya migogoro.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia Kikao cha 80 cha
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika Makao Makuu ya Umoja wa
Mataifa Jijini New York nchini Marekani. Amesema uwepo wa mitazamo ya
kibeberu, ikiwa ni pamoja na ile ya kuichukulia Afrika kuwa sehemu ya
uchukuaji rasilimali na uporaji wa ardhi, pamoja na uwepo wa makampuni
ya kimataifa kuendelea kufanikiwa kutokana na unyonyaji wa mali asili za
Afrika, huku wakisababisha au kuunga mkono migogoro inapaswa kumalizika
sasa.
Makamu wa Rais amesema Tanzania inauchukulia msimamo wa upande
mmoja na matumizi mabaya ya nguvu za kijeshi, pamoja na kushindwa kwa
jumuiya ya kimataifa na mataifa yenye nguvu duniani katika kukomesha
umwagaji damu na vita vya hatari vinavyoendelea katika maeneo mengi
duniani, kuwa ni jambo lisilokubalika.
Pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutambua kuwa ongezeko
la matumizi ya fedha katika masuala ya kijeshi ikiwemo utafiti na
utengenezaji wa silaha ni jambo la kusikitisha na ni kinyume cha
maadili. Amesema hali hiyo inazuia jitihada za kutafuta amani duniani,
na inachukua kiasi kikubwa cha rasilimali ambazo zingeweza kutumika
kuendeleza maendeleo endelevu na ustawi kwa wanadamu wote.
Makamu wa Rais amesema dunia inapaswa kuendelea kutafuta amani
bila kuchoka kwani ndio sharti la maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Amepongeza juhudi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa dunia,
na mashirika ambayo yanashiriki kikamilifu katika upatanishi na utatuzi
wa migogoro katika nchi na maeneo kama vile Mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Sudan, Urusi, Ukraine, na Mashariki ya Kati.
Ametoa wito wa ushirikishwaji kamili wa wanawake katika kutafuta amani
hususani katika kipindi hiki inaposherehekewa miaka 30 tangu azimio la
Beijing na maendeleo yaliyopatikana katika kukuza usawa wa kijinsia na
uwezeshaji wa wanawake.
Amesema Rais wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ameonyesha njia katika kueleza
sera na vitendo vinavyoimarisha nafasi ya mwanamke katika sekta zote za
jamii. Amesema kikanda na kimataifa, amekuwa mtetezi wa amani, haki,
usalama na matumizi ya nishati safi.
Amesema Tanzania kama mwanachama wa Baraza la Amani na Usalama
la Umoja wa Afrika, pia nafasi iliyotumikia kama Mwenyekiti wa Asasi ya
Siasa Ulinzi na Usalama Jumuiya ya SADC ilichangia kikamilifu katika
mipango ya amani na kuunga mkono hatua za kuzuia na kutatua migogoro.
Tanzania imetangaza kugombea kiti kisicho cha kudumu katika
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa muhula wa 2029-2030, ili
kuthibitisha dhamira iliyonayo ya amani na usalama duniani.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema, Tanzania inasisitiza
msimamo wa Afrika wa kurekebisha uwakilishi mdogo wa bara hilo katika
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kutoa wito wa kupitishwa kwa
angalau viti viwili vya kudumu vya Afrika vyenye nguvu ya kura ya
turufu.
Amesema Tanzania inaungana na nchi nyingine katika kudai
mageuzi ya haraka na ya kina ya mfumo wa fedha wa kimataifa. Ametoa wito
wa kuongeza ufadhili wa masharti nafuu wa muda mrefu, kurekebisha
mifumo huru ya ukadiriaji wa mikopo, na kufikiria upya tathmini ya
uhimilivu wa deni, ili kupatikana mtaji wa uwekezaji katika miundombinu,
elimu, afya na kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Amesisitiza nia ya
kuongezeka kwa sauti na uwakilishi wa Afrika katika miundo ya utawala ya
Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia ambayo haijafanyiwa
kazi kwa muda mrefu.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imejitolea na imepiga hatua
katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s 2030)
ikifikisha asilimia 60. Amesema kwa lengo namba 3, Tanzania imefanikiwa
kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 750 kwa kila vizazi hai
1000 mwaka 2000 hadi 104 mwaka 2022. Kwa lengo namba 6, upatikanaji wa
maji safi na salama uliongezeka katika maeneo ya vijijini na mijini
kutoka asilimia 32 na 55 mwaka 2000 hadi asilimia 79.9 na 94 mwaka 2024.
Kwa nishati safi ya bei nafuu ambayo ni lengo namba 7, Tanzania
imefanikiwa kuunganisha nishati ya umeme kwa vijiji 8,587 mwaka (2000)
hadi 12,318 mwaka 2024 ambapo ni vijiji 15 pekee vilivyobaki bila umeme.
Makamu wa Rais amehimiza jumuiya ya kimataifa kuimarisha
mwitikio wa pamoja wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Ametoa
wito wa kutumia vyema fursa ya Mkutano wa wa COP30 nchini Brazil
kuhakikisha ahadi zinatekelezwa ikiwemo uchangiaji wa Mfuko wa Hasara na
Maafa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi (Loss and Demage
Fund) pamoja na kuongezwa kwa ufadhili wa masharti nafuu wa muda mrefu,
uhamishaji wa teknolojia, na masharti ya kibiashara yanayozingatia haki
ili kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mataifa na kutafuta
ushirikiano wa manufaa kwa pande zote katika matumizi ya rasilimali.
No comments:
Post a Comment