Careen Geofrey Erneo, mmoja wa wanafunzi wa Wilaya ya Ilala, ni miongoni mwa wananchi waliojitokeza katika Ofisi ya Usajili ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuchukua Vitambulisho vyao, mara baada ya kupokea ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) uliowataka kufika ofisini hapo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Careen alieleza kuwa hatua hiyo ya kupata Kitambulisho chake kwa wakati ni jambo la kujivunia, kwani kitamrahisishia ushiriki wake katika shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na hata kielimu. Alisema kuwa Kitambulisho cha Taifa ni nyenzo muhimu kwa kijana wa kitanzania kwani ndicho kinachomtambulisha kisheria na kumfungulia fursa nyingi za kimaendeleo.
“Ninaishukuru sana NIDA kwa kuhakikisha napata Kitambulisho changu mapema. Hii imenipatia nafasi ya kuwa na uhakika katika masuala ya kitaaluma, kibenki na hata fursa za kijamii ambazo zinahitaji utambulisho rasmi. Kwa kweli, hii ni hatua kubwa kwangu kama kijana,” alisema Careen mara baada ya kukabidhiwa kitambulisho chake.
Aidha, aliwataka vijana wenzake, hususan wanafunzi, kujitokeza kuchukua vitambulisho vyao pale wanapopata taarifa kupitia SMS au tangazo lolote rasmi kutoka NIDA. Alisema kitambulisho hicho si tu kinahitajika kwa ajili ya shughuli za kila siku, bali pia ni nyenzo muhimu katika kujenga mustakabali wa maisha yao.
“Vijana wenzangu ambao bado hawajasajiliwa, nawahimiza wajitokeze kwa wingi ili wapate haki yao hii ya msingi. Kitambulisho cha Taifa ni cheti cha uraia wetu na ni sehemu ya msingi wa maendeleo yetu binafsi na ya taifa kwa ujumla,” alisisitiza.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa sasa inaendelea na jitihada za kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanapata Vitambulisho vyao, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha SMS kwa wananchi walio tayari kukabidhiwa vitambulisho vyao, ili kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa huduma na kupunguza msongamano katika ofisi zake.
No comments:
Post a Comment