Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Serikali imeongeza ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na shughuli zote za mnyororo mzima wa thamani wa madini nchini ambapo kwa Mkoa wa Geita pekee wachimbaji wadogo wamezalisha kilo 22,014.61 zenye thamani ya shilingi trilioni 3.443 na Serikali kukusanya mapato ya shilingi bilioni 2.5 katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025.
Mchango wa wachimbaji wadogo wa madini umeongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2024 katika mapato yote ya sekta ya madini na mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2024.
Akizungumza Septemba 28, 2025 katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili mkoani Geita wakati akifunga Maonesho ya Nane ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini, yenye kauli mbiu “Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Uongozi Bora/Shiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025”. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza wachimbaji wadogo na Wizara ya Madini kwa hatua hiyo.
“ Napenda kutoa pongezi maalum kwa Wizara ya Madini kwa usimamizi mzuri wa sekta hii pamoja na wachimbaji wadogo wa Tanzania. Ninyi ni sababu ya kusheherekea mafanikio haya mmekuwa shamba darasa na baada ya Serikali kuwapatia nafasi mmeonesha kwa vitu mlivyofanya mkipewa fursa mnaweza,” Amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea “Mmepambana sana kuleta teknolojia ndani ya nchi na mmeonesha Watanzania wanaweza kufanya mambo makubwa na wakafanikiwa,”
Aidha, amesema kuwa tangu kuanza kwa maonesho hayo mwaka 2018 kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia yanayochangia kuongezeka kwa kasi ya uzalishaji madini hasa kwa wachimbaji madini wadogo. Ambapo katika uchenjuaji madini, zimekuwepo teknolojia mbalimbali za kisasa zikiwemo Carbon – In – Leach (CIL), Carbon – In – Pulp (CIP) na Froth Floatation (FF) ambazo zimekuwa na tija zaidi kuliko matumizi ya zebaki ambayo imekuwa na athari nyingi za kiafya na mazingira sambamba na kiwango kidogo cha uzalishaji.
Dkt. Biteko amesema kufuatia usimamizi thabiti na mabadiliko makubwa ya teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na uwepo wa maonesho hayo ya teknolojia, Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi trilioni 3.8 kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025.
Akizungumzia hatua mbalimballi za Serikali katika kuhamasisha uongezaji thamani madini, Dkt. Biteko amesema kumekuwepo na uanzishwaji wa viwanda vya uyeyushaji na usafishaji wa madini ya dhahabu, nikeli na shaba katika maeneo mbalimbali nchini ambapo kwa sasa kuna jumla ya viwanda nane vya uchenjuaji wa shaba na nickel katika Mkoa wa Dodoma, Kiwanda kimoja cha Uyeyushaji wa Shaba (Chunya) na Viwanda Sita vya Usafishaji wa Dhahabu katika Mikoa ya Geita, Mwanza na Shinyanga-Kahama.
“ Nitoe wito kwa wachimbaji na Wizara kuendelea kubuni na kuongeza uwezeshwaji wa Watanzania kuongeza thamani ya madini wanayozalisha. Mazingira haya yataongeza upatikanaji wa fedha za kigeni pamoja na kuwapatia watanzania ajira kwenye viwanda vya uongezaji thamani, STAMICO mmefanya kazi kubwa sana kubadilisha na kushiriki kwenye local content.” Amesisitiza Dkt. Biteko.
Amewahakikishia kuwa Serikali sikivu inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya madini ikiwemo kufikisha huduma ya umeme katika maeneo yote muhimu.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewaasa washiriki wa maonesho hayo kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuwa hatua hiyo ni muhimu katika nchi ya kidemokrasia.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ambapo mwaka jana aliagiza uwanja huo wa maonesho ujengewe miundombinu ya kudumu.
Amesema agizo hilo limetekelezwa na sasa uwanja huo una mabanda tisa ya kudumu ikiwa ni awamu ya kwanza ya ujenzi.
Amesema maonesho hayo kwa mwaka huu yamehudhuriwa na washiriki 930 wakiwemo washiriki kutoka nje ya nchi ikilinganishwa na washiriki 600 mwaka 2024.
Amesema “Rais Samia amewezesha kutoa leseni 9,000 kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wa Pori la Kigosi na sasa tumeweza kuzalisha zaidi ya tani 22,000 za madini kwa wachimbaji wadogo,”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Said amewashauri wadau wa sekta ya madini kwa ujumla kutumia fursa za taasisi za fedha ili kupata elimu kuhusu masuala ya fedha na uwekezaji.
Akimwakilisha Waziri wa Madini, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema maonesho hayo yamekuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo kuwa chachu hususan kwa wachimbaji wadogo na kuwaongezea elimu kuhusu uchimbaji hatarishi na matumizi ya zebaki.
Vilevile amesema Wizara ya Madini itahakikisha inasimamia sheria na taratibu zote ili kufanya sekta hiyo kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo amesema kuwa hivi sasa sekta ya madini nchini imefikia kiwango cha kushawishi viwanda vya kuzalisha vipuri kuja kuwekeza Tanzania ili vipuri hivyo vipatikane nchini na kufikia lengo la kuwa na Tanzania ya viwanda.
Amebainisha kuwa Tume ya Madini itaendelea kuwezesha sekta ya madini ili kuhakikisha madini yanawanufaisha Watanzania wote.
Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo, Lenard Bugomola amesema kuwa Mkoa wa Geita umekuwa ukiongoza kwa uzalishaji wa dhahabu, aidha ameomba STAMICO iwapatie mitambo miwili ya uchimbaji madini.
Awali Dkt. Biteko alitembelea mabanda ya mbalimbali yakiwemo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini, Anglo Gold Ashanti, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA), Mwamba Mining ambapo alielezwa kuhusu teknolojia ya kisasa ya uchimbaji madini
No comments:
Post a Comment