Dar es Salaam, Septemba 29, 2025 – Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amempokea rasmi Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Mhe. Péter Szijjártó, katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wawili walisisitiza dhamira ya nchi zao kuendeleza na kuimarisha uhusiano wa kirafiki, kidiplomasia na kiuchumi uliodumu kwa miaka mingi. Mazungumzo ya pande mbili yalihusisha pia mawaziri na wajumbe kutoka Tanzania na Hungary, ambapo maeneo ya ushirikiano katika biashara, elimu, teknolojia, kilimo, na uwekezaji yalijadiliwa kwa lengo la kuleta manufaa kwa wananchi wa nchi zote mbili.
Mhe. Szijjártó yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja inayolenga kuimarisha mashirikiano ya kimaendeleo na kukuza fursa za kiuchumi baina ya Tanzania na Hungary. Ziara hii ni kielelezo cha uhusiano mzuri unaoendelea kujengwa na kuimarishwa baina ya pande mbili, huku ikitarajiwa kufungua njia mpya za ushirikiano endelevu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
No comments:
Post a Comment