Tuesday, September 23, 2025

TFS yaendelea kuimarisha uwezo wa wahifadhi kukabiliana na majanga ya moto













Iringa, Septemba 22, 2025 — Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kuimarisha uwezo wa wahifadhi wake kwa kuendesha mafunzo maalumu ya kudhibiti na kuzuia majanga ya moto katika mashamba ya miti nchini.

Mafunzo hayo yanayofanyika katika Shamba la Miti Sao Hill mkoani Iringa yamewakutanisha wahifadhi kutoka mashamba 24 ya miti ya kupandwa yanayosimamiwa na TFS. Yanalenga kuongeza ujuzi wa vitendo na nadharia kuhusu mbinu za kisasa za kudhibiti moto, ikiwemo utambuzi wa mapema, udhibiti wa kuenea kwa moto na matumizi ya vifaa maalumu.

Akifungua mafunzo hayo, Mhifadhi Mkuu wa Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, alisema moto wa misitu umeendelea kuwa tishio kubwa linalosababisha hasara, hivyo elimu na mafunzo ya kitaalamu ni nyenzo muhimu katika kulinda rasilimali za taifa.

“Tunahitaji kuimarisha mikakati ya kuzuia na kudhibiti matukio ya moto kabla hayajasababisha madhara makubwa. Mikakati ikitekelezwa ipasavyo, itatupa ufanisi mkubwa katika kulinda rasilimali za taifa letu,” alisema Yoramu.

Aidha, alihimiza wahifadhi kushirikiana na jamii zinazozunguka mashamba ya miti ili kuongeza uelewa wa pamoja, kuimarisha tahadhari na kuchukua hatua za haraka pindi moto unapotokea.

Kwa upande wake, Askari Mwandamizi wa Shamba la Miti Kiwila, Nassib Omary Tekelo, alisema mafunzo hayo yatasaidia wahifadhi kupata mbinu za kitaalamu na kutumia vifaa maalumu vya kudhibiti moto.

“Tunaamini elimu hii itatusaidia kulinda misitu yetu dhidi ya majanga ya moto na pia kuwaelimisha jamii zinazozunguka mashamba yetu,” alisema Tekelo.

Naye Askari Mhifadhi kutoka Shamba la Miti Buhigwe-Kasulu, Maria Lupembe, alibainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga pia kubadilishana ujuzi na uzoefu kati ya wahifadhi kutoka maeneo mbalimbali ili kurahisisha mikakati ya pamoja ya kukabiliana na majanga ya moto.

Mafunzo hayo yatakayodumu kwa siku tatu yanahusisha nadharia na vitendo, na yanalenga kuongeza mshikamano kati ya wahifadhi na jamii katika kuhakikisha usalama wa mashamba ya miti na uendelevu wa misitu nchini

No comments:

CHEREKO ZATAWALA BANDA LA REA KATIKA MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA

Furaha na shangwe (chereko) zimetawala katika Banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakati wananchi walipofurika kununua majiko ya gesi ...