Tuesday, September 30, 2025

TANAPA YAMPONGEZA SIMBU; YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NAE KUTANGAZA HIFADHI ZA TAIFA KUPITIA MCHEZO WA RIADHA










Na. Philipo Hassan, Arusha

Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji, amempongeza rasmi Sajini Taji Alphonce Simbu, bingwa wa Dunia katika mbio ndefu za kilometa 42 mwaka 2025, akisisitiza kuendelea kushirikiana naye katika jitihada za kutangaza hifadhi za taifa kupitia michezo ya riadha. Pongezi hizo zimetolewa Makao Makuu ya TANAPA, jijini Arusha, katika hafla iliyohudhuriwa na Menejimenti ya Shirika pamoja na waandishi wa habari.

Sajini Taji Simbu aliibuka mshindi wa medali ya dhahabu katika mashindano ya mbio ndefu yaliyofanyika nchini Japan kuanzia Septemba 13 hadi Septemba 21, 2025, matokeo ambayo yameipa Tanzania heshima kubwa katika jukwaa la kimataifa.

“Tunakupongeza sana Simbu kwa jitihada na bidii ulizozionyesha katika kuipambania Bendera ya Taifa letu. Ushindi huu si tu ni ushindi wa kibinafsi, bali ni utambulisho mkubwa wa taifa letu duniani,” alisema Kamishna Kuji, akiashiria umuhimu wa michezo katika kuimarisha taswira ya Tanzania kimataifa.

Aidha, Kamishna Kuji alisisitiza kuwa TANAPA iko tayari kushirikiana na wanamichezo wa kitaifa na kimataifa, si tu katika kutangaza hifadhi za taifa bali pia katika kukuza utamaduni wa michezo na maisha yenye afya. “Kupitia michezo kama mbio ndefu, wanamichezo wanakuwa mabalozi wa hifadhi zetu, wakionyesha uzuri wa maliasili na vivutio vya utalii vya Tanzania,” alisema.

Hafla hiyo pia ilijumuisha wawakilishi wa sekta ya michezo, wadau wa utalii, na waandishi wa habari, ikionyesha uwepo wa mshikamano wa jamii katika kuenzi mafanikio ya wanamichezo na umuhimu wa michezo kama njia ya matangazo ya hifadhi na taifa.

Sajini Taji Simbu, kwa upande wake, aliishukuru TANAPA kwa pongezi hizo na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa hifadhi na michezo, akisisitiza kuwa mafanikio yake ni matokeo ya jitihada za pamoja, moyo wa taifa, na msaada kutoka kwa wadau wa michezo na hifadhi nchini.

No comments:

TANAPA YAMPONGEZA SIMBU; YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NAE KUTANGAZA HIFADHI ZA TAIFA KUPITIA MCHEZO WA RIADHA

Na. Philipo Hassan, Arusha Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji, amempongeza rasmi Sajini Taji Alphonce Simbu, bingwa wa D...