Tuesday, September 30, 2025

DKT. SAMIA AHIDI KUKAMILISHA DARAJA LA PANGANI NA BARABARA YA KIMKAKATI BAGAMOYO–SAADANI–PANGANI–TANGA







Na John Bukuku, Tanga 

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuonesha dira ya maendeleo kwa Watanzania baada ya kuahidi kukamilisha ujenzi wa daraja la Pangani na barabara ya Bagamoyo–Saadani–Pangani–Tanga – miradi mikubwa itakayofungua ukanda wa Kaskazini kiuchumi na kuimarisha fursa za utalii na biashara.

Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Pangani, Septemba 29, 2025, Dkt. Samia alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 50 tayari imekamilika kwa asilimia 75, na Serikali imedhamiria kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati.

Aidha, alibainisha kuwa mara tu daraja la Pangani litakapoanza kutumika, wananchi hawatalazimika tena kusafiri umbali mrefu kuunganisha mikoa ya Pwani, Tanga na Kilimanjaro.

“Daraja la Pangani ni mkombozi wa wananchi, na barabara hii ndiyo kiunganishi muhimu cha ukanda huu. Tukikamilisha miradi hii, changamoto za usafiri zitabaki kuwa historia. Nataka kuona wananchi wa Pangani na mikoa jirani wakinufaika moja kwa moja kwa kupanuka kwa biashara, utalii na uwekezaji,” alisema Dkt. Samia huku akishangiliwa na umati wa wananchi.

Dkt. Samia alihimiza wananchi waendelee kuiamini CCM na kumpa kura ya ndiyo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili chama hicho kiendelee kusukuma mbele ajenda ya maendeleo yenye kuleta matokeo ya kweli kwa Watanzania wote.

Kwa kauli hiyo, Pangani na ukanda mzima wa Kaskazini unaendelea kupata matumaini mapya ya kimaendeleo kupitia miradi mikubwa ya miundombinu, inayolenga kuunganisha mikoa, kuongeza fursa za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

No comments:

DKT. SAMIA AHIDI KUKAMILISHA DARAJA LA PANGANI NA BARABARA YA KIMKAKATI BAGAMOYO–SAADANI–PANGANI–TANGA

Na John Bukuku, Tanga  Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hass...