Thursday, September 25, 2025

Kongresi ya 49 ya Apimondia Yafunguliwa Copenhagen; Asali ya Tanzania Yapaa Ulaya, Yaibua Fahari Apimondia










Copenhagen, Denmark — Tanzania imeendelea kuibua heshima katika sekta ya ufugaji nyuki baada ya kushiriki kikamilifu kwenye Kongresi ya 49 ya Kimataifa ya Wafugaji Nyuki (Apimondia) iliyofunguliwa Septemba 23, 2025 jijini Copenhagen, Denmark, ikihusisha zaidi ya washiriki 7,000 kutoka nchi 121 duniani.

Ujumbe wa Tanzania, ulioongozwa na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, ulihusisha pia taasisi za utafiti TaFORI, TAWIRI na TARI pamoja na wadau binafsi akiwemo Grand Apiary, Bee Topia Tanzania, PMM na Worker Bees Africa. Washiriki hao waliwasilisha tafiti, bidhaa na mikakati ya kibiashara, hatua iliyoinua hadhi ya taifa katika anga ya kimataifa.

Sambamba na kongresi hiyo, maonesho ya kibiashara ya ApiExpo yalifanyika yakihusisha kampuni 179 kutoka nchi 44, yakionesha vifaa na ubunifu mpya katika sekta ya nyuki.

Katika hotuba za ufunguzi, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dk. Qu Dongyu, na Makamu wa Rais wa Bunge la Ulaya, Martin HojsΓ­k, walisisitiza umuhimu wa nyuki katika usalama wa chakula, bioanuwai na maendeleo ya vijijini.

Septemba 24, Balozi wa Afrika Kusini nchini Scandinavia, Mhe. Fikile Sylvia Magubane, alitembelea banda la Tanzania na kusifu hatua ya nchi hiyo kuuza asali kwenye soko la Umoja wa Ulaya kwa kuzingatia viwango vya ubora. Hata hivyo, alitaka kufahamu kwa nini kongresi ijayo ya 2027 haitafanyika tena Arusha.

Akijibu, Prof. Silayo alieleza kuwa changamoto za ujenzi wa ukumbi mpya wa kimataifa (MKICC) zilisababisha Apimondia kuhamishia mkutano huo Dubai, Falme za Kiarabu.

Licha ya mabadiliko hayo, Tanzania imetajwa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika biashara ya asali, huku ikihimizwa kuendeleza ushirikiano wa kikanda ili kuimarisha nafasi ya bara hili katika soko la dunia.

No comments:

Mwili wa Hayati Askofu Mkuu Rugambwa wapokelewa Bukoba

Mwili wa Hayati Askofu Mkuu Novatus Rugambwa, aliyefariki hivi karibuni, uliwasili leo katika Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Huruma, Jimbo Ka...