Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imetembelea kijiji cha Olpiro kilichopo Kata ya Eyasi, wilayani Ngorongoro, na kuchukua hatua za kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi pamoja na mifugo yao.
Wataalam kutoka NCAA katika ziara iliyofanyika Septemba 30, 2025, wamekagua marekebisho na ukarabati wa miundombinu ya maji uliofanyika katika kijiji hicho, hatua iliyowawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.
Ukarabati wa miundombinu ya huduma ya maji katika kijiji hicho umeleta faraja kubwa kwa wananchi hao waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji kwa muda mrefu.
Aidha, pamoja na maboresho ya huduma ya maji, NCAA pia imefanya tathmini ya miundombinu mingine ikiwemo josho la kuogeshea mifugo lililopo katika kijiji hicho.
Wananchi wa kijiji cha Olpiro wameipongeza Serikali kupitia mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa jitihada hizo wakieleza kuwa zinachangia sio tu katika kuboresha maisha yao ya kila siku, bali kulinda afya zao na kuendelea kuunga mkono Serikali katika shughuli za uhifadhi.
No comments:
Post a Comment