Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Septemba 26, 2025, ametembelea familia ya marehemu Abbas Ali Mwinyi huko Bweleo, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Unguja, kuwafariji kutokana na msiba huo.
Hadi mauti ilipomkuta, marehemu Abbas Ali Mwinyi alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Fuoni, Zanzibar. Alifariki dunia jana, Septemba 25, 2025, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mjini Magharibi, Lumumba, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Ziara ya Rais Samia ilihudhuriwa pia na viongozi wengine wakuu wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, akikagua hali ya familia ya marehemu na kutoa salamu za rambirambi.
Viongozi waliokuwa pamoja na Rais Samia ni pamoja na Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dotto Mashaka Biteko; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu; Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla; Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Zuberi Ali Maulid; pamoja na Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro.
Aidha, viongozi wengine wa Serikali, chama, taasisi za umma na binafsi walijitokeza kutoa mkono wa pole, kuonesha mshikamano wa kitaifa kwa Rais Mwinyi na familia yake katika kipindi hiki kigumu.
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, mwili wa marehemu Abbas Ali Mwinyi utasaliwa katika Msikiti wa Jamia Zinjibar, Mazizini, mara baada ya Sala ya Ijumaa, na kisha kuzikwa Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, leo Septemba 26, 2025.
Msiba huu umepokewa kwa huzuni na majonzi makubwa, huku Watanzania wa pande zote za Muungano wakionesha mshikamano na mshikikano wa kitaifa kwa Rais Mwinyi na familia yake, wakiombea marehemu apumzishwe kwa amani na Mwenyezi Mungu awape wafiwa subira na moyo wa uvumilivu.
No comments:
Post a Comment