WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amekabidhi Hati za Haki Miliki za Kimila kwa wananchi 700 wilayani Ikungi mkoani Singida ambapo amewataka kuzitunza Hati hizo ili ziendelee kuwa msaada kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Januari 10, 2025, Mhe. Ndejembi amesema zoezi hilo ni muendelezo wa Serikali kupima na kumilikisha vijiji vyote nchini ikiwa ni mpango wa kumaliza changamoto ya migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.
“Hapa Ikungi kuna Vijiji 101 lakini vilivyopimwa ni 28 tu. Tayari tumeanza kuchukua hatua kwa sababu hadi kufikia 2019 ni vijiji vitano tu vilikua vimepimwa.
Niwahakikishie Wananchi wa Ikungi, nchi nzima kuna vijiji 12,300, vilivyopimwa ni kama 4,200. Kwa maelekezo ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunakwenda kupima vijiji vyote vilivyosalia katika Taifa letu ili kila kijiji kiwe kina matumizi bora ya ardhi,” amesema Mhe. Ndejembi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Mhe. Miraji Mtaturu ameishukuru Serikali kwa kupeleka kiasi cha Sh Milioni 500 kupitia mradi wa Kupanga, Kupima, Kumilikisha (KKK) ambao utasaidia kumaliza migogoro ya ardhi katika Jimbo la Ikungi.
No comments:
Post a Comment