Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (Katikati) na Balozi wa Japan nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe. Yasushi Misawa (wa tano kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja naNaibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban (wa tano kulia), Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Patrick Pima (wa nne kulia), Kamishna Msaidizi Idara ya Sera anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Masuala ya Kodi, Bw. Juma Mkabakuli (wa tatu kulia), Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Ara Hitoshi (wa nne kushoto) na Maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri
wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ametoa wito kwa
Kampuni za Japan kuwekeza nchini Tanzania ili kutumia fursa zilizopo
katika sekta mbalimbali za uzalishaji kwa faida ya pande zote mbili.
Dkt.
Nchemba ametoa rai hiyo Jijini Dodoma wakati akiagana na Balozi wa
Japan nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe.Yasushi Misawa, ambapo
pamoja na mambo mengine, alimhakikishia pia Balozi huyo kuwa Tanzania na
Japan zitaendelea kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na kijamii kwa
faida ya nchi hizo mbili.
Alisisitiza kuwa Tanzania ina fursa
nyingi za uwekezaji ikiwemo sekta ya kilimo itakayoiwezesha Tanzania
kuwa ghala la chakula lakini pia uwekezaji katika miundombinu ikiwemo
uendeshaji wa Reli ya Kisasa SGR.
Aidha, katika mazungumzo yao,
Dkt. Nchemba aliishukuru Japan kwa uwekezaji mkubwa uliochangia
maendeleo ya nchi kupitia miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na nchi hiyo
katika sekta za kilimo, afya, nishati, na ujenzi wa miundombinu
mbalimbali ikiwemo Barabara ya mzunguko katika jiji la Dodoma.
“Katika
kipindi chako pekee, tumeshuhudia Tanzania na Japan zikisaini mikataba
ya mikopo nafuu yenye thamani ya yen ya Japan bilioni 10 sawa na
shilingi za Tanzania bilioni 151 pamoja na msaada wa yen bilioni 5.5,
sawa na zaidi ya shilingi za Tanzania bilioni 83. Tunakushukuru sana na
tunakuomba uendelee kuwa Balozi mzuri wa Tanzania hata baada ya kumaliza
muda wako” Alisisitiza Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Balozi
wa Japan nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe. Yasushi Misawa,
aliyeambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan
(JICA), Bw. Ara Hitoshi, alisema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na
nchi yake umedumu kwa zaidi ya miaka 60 ambapo katika kipindi hicho,
Japan imesaidia utekelezaji wa zaidi ya miradi 360 ya kijamii na
kiuchumi.
Alibainisha kuwa baadhi ya miradi hiyo iko katika
sekta ya nishati ukiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka
Iringa hadi Shinyanga, ujenzi wa mradi wa umeme unaounganisha Tanzania
na Kenya pamoja na mpango unaoendelea kati ya Tanzania na Japan kupitia
Wizara ya Nishati wa kujenga mradi wa umeme wa joto ardhi.
Katika
mazungumzo yao ambayo yalihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya
Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban na Viongozi wengine waandamizi wa
Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, viongozi hao walijadili fursa mbalimbali za maendeleo katika
sekta za kilimo, afya, miundombinu, na kukuza uchumi na maendeleo ya
nchi kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi pamoja
na uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment