Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amepongeza juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya afya nchini, akisema dhamira yake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za uhakika bila kulazimika kuzifuata nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Afya Kizimkazi, Wilaya ya Kusini Unguja, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Balozi Kombo alisema, "Vission yake ni kwamba wasitoke wagonjwa kutoka Zanzibar kwenda kutibiwa nje ya nchi. Watatibiwa hapa hapa, huo ndiyo muono wake."
Alifafanua kuwa ujenzi wa Kituo cha Afya Kizimkazi ni sehemu ya mpango mkubwa wa Samia Foundation unaolenga kuboresha huduma za afya nchini. "Hiki Kituo cha Kizimkazi ni asilimia ndogo sana ya mpango mzima wa Mama Samia Foundation, lakini muundo na vission yake ni kubwa zaidi," alisema.
Balozi Kombo alieleza kuwa yeye pamoja na Dkt. Jakaya Kikwete walipewa jukumu maalum la kwenda kujifunza mifumo ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute ili kuimarisha utekelezaji wa mpango huu. Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza Mhandisi aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Samia Foundation, akisema uteuzi huo utasaidia kutafsiri ndoto pana ya Rais Dkt. Samia kwa manufaa ya Watanzania wote.
Akizungumzia hatua za maendeleo katika sekta nyingine, Waziri Kombo aliipongeza serikali ya Rais Samia kwa kuwekeza katika upatikanaji wa nishati ya uhakika, hatua ambayo imeungwa mkono na viongozi wa ndani na nje ya Afrika.
Kituo cha Afya Kizimkazi kinatarajiwa kuwa mfano wa miradi mingine itakayotekelezwa chini ya Samia Foundation ili kuimarisha ustawi wa wananchi na kupunguza mzigo wa kutafuta matibabu nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment