Na Beatus Maganja, Malinyi
Mkuu
wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba amesema zoezi la kuwalipa
fidia wananchi wa Kijiji cha Ngombo kilichopo ndani ya Pori la Akiba
Kilombero Mkoani Morogoro linaendelea vizuri ambapo asilimia 93 ya
wananchi wote tayari wamekwishalipwa fidia zao kwa ajili ya kupisha
shughuli za uhifadhi katika Hifadhi hiyo na asilimia 7 ya wananchi
waliosalia wanaendelea kushughulikiwa ili kukamilisha malipo yao.
Akizungumzia
zoezi hilo jana Desemba 31, 2024 wilayani humo Mhe. Sebastian amesema
Serikali imetoa zaidi ya shilingi billioni 6.9 kulipa wananchi 1,056 ili
waweze kuhama kwa hiari kutoka maeneo ya Hifadhi huku akitoa maelekezo
kwa watendaji wa vijiji 32 wilayani Malinyi kuwapokea ili waweze
kuendelea na shughuli zao za kila siku.
“Kwanza
si kweli kwamba wananchi wa Ngombo hatujawaambia mahali pakwenda.
Katika barua yangu ya tarehe 4 Disemba, 2024 niliyowaandikia watendaji
wa vijiji 32 vilivyo ndani ya wilaya ya Malinyi, nilitoa maelekezo ya
kuwapokea wananchi wa Kijiji cha Ngombo wanaopisha shughuli za uhifadhi
katika Pori la Akiba Kilombero, na ndivyo inavyofanyika na pia
nilielekeza watendaji hao wawataarifu wananchi wote kupitia mikutano ya
hadhara” amesema
“Na
tangu wananchi wangu wa Ngombo walipoanza kuhama kwenda katika maeneo
yao waliyokwenda, sijapata lalamiko lolote kwa simu au kwa mdomo kwamba
wamezuiliwa kukaa mahali fulani na kwa taarifa nilizonazo baadhi yao
wamehamia sehemu mbalimbali ikiwemo Mikoa ya Lindi, Ruvuma, Pwani na
Halmashauri ya Mlimba. Kwahiyo mimi ninaamini mambo yanakwenda vizuri na
ndivyo ilivyo” amesisitiza Sebastian.
Kuhusu
wanafunzi waliokuwa wanasoma shule katika Kijiji cha Ngombo, Mkuu huyo
wa wilaya amesema amekwishatoa maelekezo kwa Afisa elimu kuwapokea na
kuwasajili katika shule zilizopo kwenye vijiji vilivyo ndani ya wilaya
hiyo bila masharti yoyote ili waweze kusoma kwa uhuru.
Aidha,Sebastian
amesema wananchi wa Kijiji cha Ngombo waliandaliwa mapema kwa kupewa
elimu juu ya malipo ya fidia ili weweze kuhama kutoka katika eneo la
Hifadhi ya Kilombero tangu mwezi Agosti, 2024. Hivyo, walikuwa na uelewa
kuhusu zoezi hilo na amewataka kuepuka watu wenye nia ovu ya kupotosha
dhamira njema ya zoezi hilo.
Kwa
upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Biro Elizabeth Mnenuka amekiri
kupokea zaidi ya wananchi 50 katika Kijiji cha Biro na wengine zaidi ya
30 katika Kijiji cha Mbalinyi na kuongeza kuwa baadhi yao tayari
wameshapatiwa maeneo kwa ajili ya kuendeleza kwa kilimo na makazi.
Nao
wananchi waliohamia Kijiji cha Biro kutoka Kijiji cha Ngombo
wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa
kuwalipa fidia zao Kwa wakati ambazo zimewasaidia kuhama na kuanza
maisha mapya katika vijiji jirani.
“Toka
nitoke Kijiji cha Ngombo ambapo tuliondolewa kisheria kwakweli sina
changamoto yoyote kimaisha, niko vizuri naishi vizuri na familia.
Naishukuru Serikali, fidia nimepata kwahiyo mpaka hapa sina neno na
Serikali” amesema Daudi Deodatus Lyambu aliyekuwa mkazi wa Ngombo ambaye
sasa amehamia Kijiji cha Biro.
Ikumbukwe
kuwa mnamo tarehe 17 Februari, 2023 Pori la Akiba Kilombero lenye
sehemu A na B lilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 64 kufuatia
kupandishwa hadhi kwa sehemu ya Pori Tengefu la Kilombero kuwa Pori la
Akiba.
Aidha,
kufuatia kuanzishwa kwa Pori la Akiba Kilombero, masharti na sheria
zinazosimamia eneo hilo zilibadilika ambapo shughuli zote za kibinadamu
zimesitishwa isipokuwa zile zinazokubalika kwa mujibu wa sheria. Lengo
la Serikali likiwa ni kuimarisha usimamizi wa eneo hilo kwa kuhifadhi
vyanzo vya maji, misitu na wanyamapori ili kuongeza tija ikiwemo
upatikanaji wa maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme katika Bwawa la
Mwl. Nyerere.
No comments:
Post a Comment