JKCI imefungua tawi jipya katika jengo la Oyster Plaza
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefungua tawi jipya kuwapa wananchi nafasi kuwa karibu na huduma ili pale wanapopata changamoto za kiafya wasichukue muda mrefu kufuata huduma zilipo.
Tawi hilo lililopo katika jengo la Oyster Plaza Haile Salassie barabara ya Ali Bin Said limeanza kutoa huduma bobezi za moyo leo lengo likiwa kuwapa fursa wananchi kupata huduma katika maeneo tofauti na ilipo taasisi hiyo na kupunguza msongamano uliopo katika makao makuu ya taasisi
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imekuwa ikiwafikia wananchi walipo kwa kuwafuata mikoani na kuwapa huduma bobezi za uchunguzi na matibabu ya moyo.
“Tumekuwa tukiwafuata wananchi mikoani kuwapa huduma sasa tumeamua kuanzisha matawi ya Taasisi, hii pia ni sehemu ya kuwafuata wananchi mahali walipo kwani hapa tulipo leo tunawapa nafasi wananchi wa eneo hili kupata huduma kwa karibu lakini pia hata wale wanaotoka mbali tunawapa nafasi ya kupunguza msongamano uliopo makao makuu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema JKCI pia inaendelea kuyafikia makundi ya watu mbalimbali kuwapa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo ili makundi yote yanayofikiwa yaweze kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao na kuwa na tabia za kuchunguza afya zao mara kwa mara.
“Tumekuwa tukiwafikia watu tofauti kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo, kipindi hiki cha kufunga mwaka tunatoa huduma kwa wasanii, na wanamichezo kila jumamosi na jumapili katika kliniki yetu ya Kawe, wanahabari tulishawapa huduma hii huko nyuma ila tutakuja kuwarudia tena”
Aidha Dkt. Kisenge ametoa wito kwa wasanii na wanamichezo kuendelea kujitokeza kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwani kinga ni bora kuliko tiba na kama watagundulika mapema watakuwa kwenye nafasi ya kutibiwa magonjwa hayo mapema na kupona.
Kwa upande wake mwananchi aliyepatiwa huduma katika kliniki ya JKCI iliyopo Oyster Plaza Haile Salassie ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuwa na maono ya kusogeza huduma karibu na jamii na kuipa jamii ari ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo.
Mwananchi huyo ambaye hakutaka jina lake lifahamike alisema huduma za afya zikiwa karibu na jamii zinatoa motisha kwa jamii kufika hospitali na kufanya uchunguzi wa afya hivyo kupunguza matumizi ya dawa yasiyo sahihi.
“Mara nyingi tumekuwa tukipata hali za maumivu ama kuumwa kichwa, mafua, kikohozi, kifua tunaenda duka la dawa kununua dawa tu bila ya kufanya uchunguzi lakini kama tutakuwa karibu na Hospitali itatusaidia kwenda kupima kwanza na kupata ushauri wa daktari kabla ya kununua dawa”, alisema.
Naye msimamizi wa kliniki hiyo Nyanjura Nyaruga alisema kliniki hiyo imeanza kwa kuwa na mwitikio mkubwa wa watu waliofika kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Nyanjura ambaye pia ni Afisa Muuguzi mbobezi wa magonjwa ya moyo alisema katika kliniki hiyo wanatoa huduma za kliniki ya moyo, kliniki ya mishipa ya damu, kliniki ya magonjwa ya moyo kwa watoto, huduma za maabara, huduma za mazoezi kwa wagonjwa wa moyo na huduma za dharura.
“Wananchi wasisite kufika katika kliniki yetu hii kwani tumejipanga kufikisha huduma bora kwenu na tutakuwa tukitoa huduma zetu kwa muda wa masaa ishirini na nne”, alisema Nyanjura
Comments