Friday, January 10, 2025

MAKAMU WA RAIS: TANZANIA INAENDELEA KUTHAMINI USHIRIKIANO NA MAREKANI









Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, amepongeza ushirikiano thabiti kati ya Tanzania na Marekani, ambao umechangia maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, biashara, na teknolojia.

Akizungumza katika mazungumzo ya kumuaga Balozi wa Marekani nchini, Mheshimiwa Michael Battle, yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, Makamu wa Rais alibainisha mafanikio makubwa yaliyotokana na ushirikiano huo. Alitaja programu kama Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), huduma za afya ya mama na mtoto, na Programu ya M-Mama kama mifano ya mafanikio hayo.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa Tanzania inatarajia kuimarisha uhusiano huo kwa kushirikiana na Balozi ajaye wa Marekani. Alieleza kuwa maeneo yanayolengwa ni pamoja na kukuza biashara kati ya mataifa hayo mawili, kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Marekani hadi Tanzania kwa ajili ya kukuza utalii, na kuimarisha ushirikiano katika teknolojia ili kuchochea maendeleo ya kilimo na nishati safi ya kupikia.

Aidha, alitaja umuhimu wa ushirikiano katika sekta ya elimu kwa kutoa mafunzo kwa vijana na kujenga rasilimali watu yenye uwezo wa kuharakisha maendeleo ya taifa.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais alitoa salamu za pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa 39 wa Marekani, Hayati Jimmy Carter, akisema dunia imepoteza kinara wa demokrasia na amani. Pia, alituma salamu za pole kwa wahanga wa janga la moto lililotokea Los Angeles, Marekani.

Kwa upande wake, Balozi Michael Battle alishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano alioupata wakati wa muhula wake, na kuahidi kuwa Balozi ajaye ataendeleza mafanikio yaliyopatikana. Alielezea programu ya “R” Nne ya Rais Samia Suluhu Hassan kama alama ya mageuzi ya maendeleo na utawala bora.

Mazungumzo haya yalihitimisha muhula wa Balozi Battle nchini, huku yakidhihirisha dhamira ya kuendelea kukuza uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Marekani.

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais

Chamwino, Dodoma


No comments:

MAKAMU WA RAIS: TANZANIA INAENDELEA KUTHAMINI USHIRIKIANO NA MAREKANI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, amepongeza ushirikiano thabiti kati ya Tanzania na Marekan...