Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akilihutubia Taifa wakati akitoa Salaam za kuaga Mwaka 2024 na kuukaribisha Mwaka mpya wa 2025 Ikulu ndogo Tunguu Zanzibar tarehe 31 Desemba, 2024.
Ndugu Wananchi;
Leo,
tarehe 31 Disemba, tunauhitimisha mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka 2025.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, kwa neema ya uhai na afya njema. Wapo
wenzetu wenye changamoto za kiafya, ambao tunaendelea kuwaombea kwa
Mwenyezi Mungu awajaalie afya njema ili warudi kwenye shughuli zao za
kujenga Taifa.
Kuna ndugu na jamaa zetu ambao tungetamani
kuwa nao leo hii, lakini kwa mapenzi yake Mola, haikuwezekana. Tuendelee
kuwaombea mapumziko mema peponi. Amen
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2024 ulikuwa mwaka wa kihistoria, wenye mafanikio na unaotupa
matumaini zaidi tunapoitazama kesho ya Taifa letu. Katika jitihada za
kutekeleza majukumu yangu, nilipata fursa ya kufanya ziara katika baadhi
ya Mikoa, na kote nilikopita nimejionea ari na hamasa kubwa ya wananchi
kujiletea maendeleo. Kuanzia Morogoro hadi Rukwa, Mwanza hadi Ruvuma na
Zanzibar, kote niliona kazi inaendelea. Serikali inatekeleza majukumu
yake, wananchi wanajituma na mabadiliko yanaonekana.
Leo
nitagusia baadhi ya masuala makubwa yaliyojiri mwaka tunaoumaliza,
changamoto tulizokabiliana nazo na tunayoyatarajia mwakani 2025.
Ndugu zangu;
Kama nilivyotangulia kusema kuwa mwaka 2024 ulikuwa ni wa
kihistoria. Tuliadhimisha miaka 60 ya kuasisiwa kwa Muungano wetu. Kama
alivyowahi kusema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere “Tanzania ni
nchi ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe, baada ya
kukomboa sehemu zake kutoka katika Ukoloni.” Hivyo basi, tuendelee
kujivunia na kuudumisha Utaifa wetu, uliojengwa katika misingi imara ya
Muungano wa Jamii mbili zenye udugu wa asili.
Pamoja na
kuadhimisha miaka 60 ya Muungano, tuliadhimisha pia miaka 60 ya
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania, miaka 60 ya Jeshi la Polisi, na miaka 60 ya Mbio za Mwenge
wa Uhuru.
Ni fahari kwamba tulifanya maadhimisho hayo yote
huku nchi yetu ikiwa salama yenye Amani na Utulivu. Kwa hakika,
ninavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanayoifanya
ya kulinda nchi yetu. Nawashukuru pia wananchi kwa kuendelea kudumisha
amani na umoja wa kitaifa; umoja ambao unaifanya Tanzania kuwa na sifa
ya kipekee.
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu pia tulikuwa
na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika kwa amani na utulivu.
Katika uchaguzi ule, kwa mara ya kwanza, wagombea ambao hawakuwa na
washindani ilibidi wapate ridhaa ya wananchi, kwa kupigiwa kura ya ndiyo
au hapana. Hii imeondosha rasmi utaratibu wa kupita bila kupingwa,
ambayo ni hatua kubwa katika ujenzi wa demokrasia nchini.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2024 ulikuwa wenye neema na mafanikio, hatuna budi kumshukuru
Mungu kwa yote. Uchumi wa nchi yetu uliendelea kuimarika na
kuwanufaisha wananchi. Kati ya Januari hadi Juni 2024 uchumi ulikua kwa
asilimia 5.4 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho
mwaka 2023. Deni la Taifa nalo liliendelea kuwa himilivu. Mfumuko wa bei
umebaki ndani ya lengo la asilimia 3, hali iliyochangiwa na sera
madhubuti za kifedha.
Tulishuhudia ongezeko la uwekezaji
kutoka ndani na nje ya Nchi. Kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania kati
ya Januari hadi Novemba 2024, tumesajili miradi ya uwekezaji 865 yenye
thamani ya Dola za kimarekani bilioni 7.7 inayotarajia kuzalisha ajira
205,000.
Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo
ya Nje (EPZA), imetoa vibali vya kuwekezwa nchini viwanda vipya vikubwa
15 vyenye thamani ya Dola za Marekani milioni 235, vinavyotarajia
kuzalisha ajira karibu 6,000 na kuuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola
za kimarekani milioni 94 kwa mwaka.
Kwa upande wa mapato,
Mamlaka ya ukusanyaji Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya
Shilingi trilioni 21.276 kati ya mwezi Januari na Oktoba, 2024 sawa na
asilimia 99.3 ya lengo. Hili ni ongezeko la asilimia 17.5 ikilinganishwa
na makusanyo katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Mwaka
huu pia tumeendelea na jitihada za kujenga uchumi wa kidijitali kupitia
matumizi ya TEHAMA. Katika kufanikisha hilo, tumeunda Wizara mahsusi ya
TEHAMA na tayari tumezindua Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali. Miongoni
mwa mipango yetu ya baadaye katika kutekeleza mkakati huo ni kuhakikisha
kuwa kila Mtanzania anatambulika kwa kutumia Jamii Namba, itakayotolewa
na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa Diplomasia, mwaka huu nchi yetu ilizidi kuimarika na
kutuletea manufaa makubwa katika nyanja za kimataifa. Tumepata heshima
ya kushiriki Mkutano wa G20, ambao pamoja na maamuzi mengine
yaliyofanyika, mkutano huo pia uliazimia kuunga mkono jitihada za
upatikanaji wa nishati safi, na vile vile, uliazimia kuimarisha
uwekezaji kwenye kilimo ili kuondosha njaa na umaskini duniani; jitihada
zinazoendana na malengo yetu Tanzania.
Kwa mara nyingine
tena, Tanzania iling'ara kwenye medani za kimataifa baada ya mgombea
wetu Mheshimiwa Daktari Faustine Ndugulile kuwania na kushinda nafasi ya
kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika. Hata
hivyo, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Ndugulile alituacha
kabla hata ya kuingia ofisini. Tunazidi kumuombea pumziko la Amani.
Ndugu Wananchi,
Ziara tulizozifanya katika nchi 16 duniani, zilituwezesha kujenga
mahusiano ya kidiplomasia, na kiuchumi. Ziara yangu nchini Jamhuri ya
Korea, ilifanikisha kupatikana fedha zenye masharti nafuu kiasi cha
Dola za kimarekani bilioni 2.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi katika
sekta za maendeleo. Kupitia fedha hizo, pamoja na mambo mengine,
tutajenga kituo cha kisasa cha mafunzo ya reli, chuo cha mafunzo ya anga
na urubani, ujenzi wa kituo cha kusambaza umeme Nyakanazi, na kituo cha
uchenjuaji wa madini na maabara za kisasa za vito.
Miradi
mingine itakayoangaliwa ni mradi wa Uendelezaji wa Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili, Ujenzi wa Kongani ya Viwanda Bagamoyo, na Ununuzi wa
Mabehewa ya Abiria na Mizigo kwa ajili ya Kipande cha Reli kutoka Mwanza
hadi Isaka, Ujenzi wa Bandari ya Wete na Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi
Bagamoyo. Fedha hizo pia zitatumika kwenye Ujenzi wa Barabara Zanzibar,
ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano Zanzibar, na Ujenzi wa Studio ya Filamu ya
Kisasa na Kituo cha burudani mbalimbali kwa ajili ya ajira za vijana.
Ziara hiyo pia ilifanikisha kusainiwa kwa Mkataba wa masharti nafuu
wenye kiasi cha Dola za Marekani milioni 163.6 kwa ajili ya kugharamia
mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Binguni na Kituo cha Mafunzo ya Afya
huko Zanzibar.
Ziara ya nchini China, pamoja na kuimarisha
uhusiano wa kidiplomasia, ilifungua milango ya soko la bidhaa mbalimbali
ikiwemo mihogo mikavu, soya, mabondo ya samaki, mazao ya baharini,
asali, mashudu ya alizeti na pilipili. Ni matarajio yangu kuwa wakulima
na sekta binafsi watachangamkia fursa hizi ili tuweze kunufaika na soko
hilo. Wakati wa ziara hiyo, Tanzania, China na Zambia zilikubaliana
kuifufua reli ya TAZARA ili kuboresha usafiri wa abiria na usafirishaji
wa mizigo.
Kwa upande wa ukanda wa SADC tulipata heshima ya
kupokea Uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika, yenye jukumu la kusimamia masuala ya Ulinzi
na Usalama katika Kanda hiyo, ambapo mbali na masuala mengine tumeweza
kusimamia uangalizi wa chaguzi kwenye Nchi za Botswana, Mauritius,
Msumbiji na Namibia.
Ndugu Wananchi,
Kuimarika kwa
uchumi kumetuwezesha kuendelea kufanya mabadiliko chanya katika mifumo
yetu wa Elimu Msingi na Sekondari hadi vyuo vya ufundi. Tumeendelea
kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi, kutandaza zaidi
miundombinu ya umeme, na kusambaza umeme vijijini. Aidha, tumetekeleza
dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani, kwa kusimamia utekelezaji wa
miradi 1,300 ya maji nchi nzima. Kukamilika kwa miradi hio kutatufikisha
kutimiza lengo la asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.
Katika sekta ya kilimo tulifanikiwa kuhamasisha kuongeza
uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, kuboresha mifumo ya masoko
ya mazao mbalimbali, na kupata bei nzuri ya mazao kwa wakulima. Kwa
mfano, kwa mwaka 2024 ufuta uliuzwa kwa Shilingi 4,850 kwa kilo
ikilinganishwa na Shilingi 3,600 mwaka uliopita 2023; Kahawa aina ya
Arabika iliuzwa kwa Shilingi 8,500 kwa kilo ikilinganishwa na Shilingi
6,500 mwaka uliopita na kwa kahawa aina ya Robusta iliuzwa kwa Shilingi
5,000 kwa kilo badala ya shilingi 3,500 mwaka 2023. Mbaazi iliuzwa kwa
Shilingi 2,236 kwa kilo mwaka 2024 badala ya Shilingi 2,000 mwaka 2023,
kakao imeuzwa kwa Shilingi 35,000 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya
Shilingi 29,500 mwaka uliopita 2023; na korosho iliuzwa kwa Shilingi
4,195 mwaka 2024 ikilinganishwa na Shilingi 2,190 mwaka 2023, huku
uzalishaji wa korosho unatarajiwa kufikia tani 425,205 kwa msimu wa
2024/2025 unaoendelea ikilinganishwa na tani 310,787 zilizozalishwa
msimu uliopita wa 2023/2024.
Mwelekeo wa Serikali ni
kuboresha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kupitia soko la Bidhaa Tanzania
(TMX) kwa mazao ya kilimo.
Ndugu Wananchi,
Tukiangazia miradi ya kimkakati, baadhi yake tayari imefikia hatua ya
kuanza kutoa huduma. Bwawa la Mwalimu Nyerere limeanza kuzalisha umeme,
na kufanya hali ya huduma za umeme nchini kuimarika. Uzalishaji kwa sasa
umefikia jumla ya Megawatt 3,169 ikilinganishwa na mahitaji ya Megawatt
1,888.
Aidha, Mradi wa Reli ya Kisasa - SGR, unatoa huduma
kutoka Dar es Salaam kupitia Morogoro hadi Dodoma. Shirika la Reli
lilikuwa linasafirisha wastani wa abiria laki 3 hadi 4 kwa mwaka.
Inafurahisha kwamba ndani ya miezi mitano ya huduma za SGR, zaidi ya
abiria 1,200,000 wameshasafiri na reli hiyo.
Tumeendelea na
maboresho kwenye sekta ya anga na uwekezaji kwenye shirika la ndege
Tanzania. Mwaka huu, Shirika letu limefikisha ndege 16, na limeongeza
safari za ndani ya nchi na kimataifa kufikia 25, ikiwemo kuanza tena
safari za abiria kwenda Afrika Kusini na kukamilisha taratibu za kuanza
safari za mizigo kwenda China. Mwaka huu Shirika limefanikiwa
kusafirisha abiria zaidi ya milioni 1 na laki 1 na zaidi ya tani 10,000
za mizigo.
Serikali pia imeendelea kuwekeza kwenye
miundombinu ya anga na kuboresha mifumo kwenye viwanja vya ndege. Mwaka
huu tuliendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Arusha, Kahama,
Mpanda, na Songwe. Mwakani tunatarajia kukamilisha viwanja vya ndege vya
Iringa, Mtwara, Songea, Kigoma, Msalato, Musoma, Shinyanga na
Sumbawanga.
Hapa nataka nisisitize kuwa, miradi hii
ni yetu sote, na imejengwa kwa kutumia rasilimali zetu. Hivyo,
tunawajibika kuitunza ili itunufaishe sisi na vizazi vijavyo kesho.
Vitendo vya kuhujumu miradi hii ni kulihujumu Taifa.
Ndugu Wananchi,
Katika
hatua nyingine, tuliendeleza mageuzi ndani ya Serikali ili kuimarisha
utendaji na ufanisi. Tuliendelea na zoezi la kubaini taasisi na
mashirika yanayopaswa kufutwa, kuunganishwa au kurekebishwa kwa lengo la
kuongeza tija na ufanisi zaidi.
Mwaka huu pia tuliendelea
kuchukua hatua za kuimarisha sekta ya ushirika ili kuchochea maendeleo
vijijini. Dhamira ya Serikali ni kurejesha hadhi ya ushirika nchini.
Ili kupata maendeleo endelevu kwa ushirika na wana-ushirika, Serikali
imechagiza mchakato wa kuanzisha Benki ya Ushirika, ambayo iko katika
hatua za mwisho, ikiwemo kufikia lengo la ukwasi wa shilingi bilioni 50.
Mwaka huu tuliendelea kushirikisha sekta binafsi na
kuhamasisha uwekezaji kwa njia ya ubia baina ya Serikali na Sekta
Binafsi (PPP) ili kuongeza ufanisi katika sekta za uzalishaji na huduma.
Katika kufanikisha hilo mpaka sasa kuna jumla ya miradi 74 ya Ubia
ambayo ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi na utekelezaji. Hadi
kufikia mwezi Desemba 2024, miradi 4 imefikia hatua ya utekelezaji,
ambapo miradi miwili 2 ni ya uendeshaji wa bandari inayosimamiwa na TPA.
Miradi mingine ni Ujenzi wa Jengo la Biashara (Business Complex) kubwa
kuliko zote Kariakoo na ule wa Ubungo - East African Logistic.
Miradi mingine inayotazamiwa kuanza utekelezaji mwakani 2025 ni
ujenzi wa barabara ya Haraka (Express way) kutoka Kibaha- Chalinze - km
78.9, mradi wa Ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto chini ya Shirika la
Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi, mradi wa mabasi yaendayo kwa haraka
(BRT) chini ya DART na mradi wa Ujenzi wa Jengo la Biashara na Hoteli ya
Nyota Nne katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere chini ya Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Ndugu Wananchi,
Katika kukabiliana na athari za mazingira kutokana na matumizi ya kuni,
mwaka huu tulizindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia.
Niwatake wahusika wasimamie ipasavyo utekelezaji wa Mkakati wa kuchochea
matumizi ya nishati safi ili kufikia lengo la asilimia 80 ifikapo mwaka
2034. Aidha, nitoe rai kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa zitokanazo
na kukua kwa matumizi ya nishati safi.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na kuwa ni mwaka wa kihistoria na mafanikio, mwaka 2024 pia
ulikuwa na changamoto zake. Nitagusia zile kubwa na namna
tulivyokabiliana nazo.
Changamoto moja kubwa
tuliyokabiliana nayo ilikuwa ni athari za mvua za El Nino na Kimbunga
Hidaya, iliyosababisha mafuriko, maporomoko na upotevu wa maisha,
uharibifu wa makazi, mashamba na baadhi ya miundombinu ikiwemo barabara
na madaraja sehemu mbali mbali nchini. Tulisimama pamoja kama Taifa,
misaada ya kibinadamu kwa waathirika kama vile vifaa vya ujenzi,
chakula, nguo na malazi ilitolewa. Aidha, Serikali ilijenga nyumba 109
kwa ajili ya walioathirika na maporomoko kule Manyara.
Kupitia TANROADS na TARURA, Serikali ilitumia shilingi bilioni 136
kutengeneza miundombinu iliyoathiriwa. Pia tulitenga shilingi bilioni
868 kutekeleza miradi 70 ya kujenga miundombinu katika maeneo
mbalimbali yaliyoathiriwa. Ni wazi kuwa, nguvu kubwa iliyotumika
kushughulikia changamoto hiyo ya dharura iliathiri utekelezaji wa baadhi
ya miradi ya barabara iliyokuwa inaendelea katika maeneo mbalimbali
nchini.
Changamoto nyingine kubwa tuliyokabiliana nayo
mwaka huu ilikuwa ni uhaba wa fedha za kigeni, hususan Dola ya Marekani.
Hali hii iliathiri shughuli nyingi za biashara na uzalishaji. Katika
kukabiliana na athari hizo, tuliunda kikosi kazi cha wataalam
kilichotafiti hali hio na kushauri hatua za kuchukuliwa. Ushauri
ulituongoza kutengeneza Mkakati wa Taifa wa Kuimarisha Upatikanaji wa
Fedha za Kigeni. Nafarijika kwamba, kufuatia utekelezaji wa Mkakati huo,
upatikanaji wa fedha za kigeni umeimarika. Aidha, katika kuchukua
hatua za kuuhami uchumi wetu, Serikali imefanya uamuzi wa kuweka akiba
ya taifa ya dhahabu katika Benki Kuu ya Tanzania, ili kuongeza uhimilivu
wa uchumi wetu.
Katika mwaka 2024, nchi yetu ilikumbwa na
jinamizi la ajali za barabarani. Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania
zinaonesha kuwa kati ya Januari hadi Disemba mwaka huu, nchi yetu
ilishuhudia jumla ya ajali 1,735. Na ajali 1,198 kati ya hizo
zilisababisha vifo vya ndugu zetu 1,715. Hii ni idadi kubwa sana. Ndugu
zetu wengine 2,719 walijeruhiwa katika ajali za barabarani. Asilimia 97
ya ajali hizi zimetokana na makosa ya kibinadamu, kubwa kabisa ikiwa
uzembe wa madereva, uendeshaji hatari na mwendo kasi ambayo kwa pamoja
ni asilimia 73.7% ya ajali zote. Niwatake Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi na Jeshi la Polisi Tanzania kuongeza mikakati ya kuzuia ajali
zinazosababishwa na makosa ya uzembe.
Ndugu zangu,
Katika kutatua changamoto hizo nilizoziainisha, tumedhihirisha
uwezo wetu Kitaifa wa kukabili changamoto zinazojitokeza. Ninawashukuru
sana wananchi wote kwa ustahimilivu, ushirikiano na uelewa wenu
tunapopatwa na changamoto za aina hio. Hakika, tunauaga mwaka huu,
tukiwa na faraja zaidi kwamba hakuna changamoto tuliyoshindwa kuikabili
tunaposimama pamoja kama Taifa.
Ndugu Wananchi;
Kama mlivyosikia, pamoja na changamoto tulizokabiliana nazo, mwaka
tunaoumaliza, umekuwa wa mafanikio mengi yanayoimarisha ustawi wa
wananchi. Katika mwaka tunaouanza muda mchache ujao, Serikali yetu
itaendelea kuimarisha na kusambaza huduma za kijamii (Afya, Elimu, Maji
na Umeme), tutachochea maendeleo kupitia ujenzi wa miundombinu,
kuwaongezea fursa vijana na wanawake katika Biashara ndogo na za kati,
na kuimarisha ustahimilivu wa Taifa.
Tutaendelea
kukamilisha miradi ya kimkakati, ikiwemo Bwawa la Kuzalisha Umeme la
Mwalimu Nyerere, Daraja la Kigongo/Busisi ambalo limefikia asilimia 94,
linalotazamiwa kulikamilisha mwezi Februari, 2025. Tutatoa kipaumbele
katika utekelezaji wa miradi ya kupunguza msongamano katika miji mikubwa
kama vile Jiji la Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma na
kurahisisha usafiri na usafirishaji katika miji inayokua kwa kasi.
Miongoni mwa miradi hii ni mradi wa Barabara za Mzunguko katika
Jiji la Dodoma ambao umefikia asilimia 80, upanuzi wa Barabara ya
Uyole-Ifisi-Songwe Airport jijini Mbeya ambao umefikia asilimia 20, na
Awamu ya Tatu na Nne ya miundombinu ya barabara za mwendo kasi jijini
Dar es Salaam, huku tukianza huduma kwenye Awamu ya Pili kwa njia ya
Mbagala iliyokwishakamilika.
Mapema mwakani, tunatazamia
Reli ya SGR, ianze kusafirisha mizigo kwa vipande vya Dar es Salaam hadi
Dodoma kiasi cha tani milioni 1 kwa mwaka, lengo ni kukuza ushoroba wa
kibiashara na kimaendeleo unaochochea uzalishaji na ajira kwa wananchi
kote inapopita. Vile vile, tutakamilisha kipande cha Mwanza hadi Isaka
na kukifanya kianze kutoa huduma. Ujenzi wa vipande vyengine hadi
Kigoma vitaendelea kujengwa kama ilivyopangwa.
Ndugu Wananchi,
Katika
juhudi za kuvutia Michezo na Mikutano ya Kimataifa, Serikali itajenga
viwanja na maeneo yenye sifa za Kimataifa kwa ajili hiyo. Mbali na
ukarabati mkubwa unaofanywa katika viwanja vya mpira wa miguu vilivyopo,
nchi yetu inaendelea kujenga viwanja vyengine kule Arusha na Dodoma.
Kama mnavyofahamu mwezi Februari 2025, nchi yetu inatarajiwa kuwa
mwenyeji wa mashindano ya CHAN na mwaka 2027 kutachezwa mashindano ya
AFCON. Sambamba na miundombinu ya michezo tumeanza jitihada za kujenga
na kurekebisha kumbi za mikutano katika viwango vya kimataifa ili tuweze
kuvuta mikutano mingi zaidi. Kwa kuwa nchi yetu imebeba ajenda ya
upatikanaji wa nishati safi Afrika, tumepata heshima ya kuwa wenyeji wa
Mkutano kuhusu masuala ya nishati kwa Bara la Afrika (Africa Energy
Summit) unaoandaliwa kwa ushirikiano wa Benki ya Dunia na Benki ya
Maendeleo ya Afrika utakaofanyika mwezi Januari 2025.
Ndugu Wananchi,
Nchi yetu imeendelea kusimamia utekelezaji wa Falsafa ya R4,
inayohimiza Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga nchi yetu. Vile
vile, tunaendeleza uhuru wa habari unaoashiriwa na idadi kubwa ya
vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, na uhuru kutoa maoni kupitia
vyombo mbalimbali; na hata uhuru wa kukusanyika na kujumuika.
Tutaendeleza
mchakato wa kupata maoni ya Wananchi ili tukamilishe uandishi wa Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2025 mapema mwakani ili tuanze utekelezaji wake.
Niwapongeze wananchi wote waliochangia katika mchakato huu, na niwasihi
tuendelee kutoa maoni yetu hadi mchakato utakapokamilika.
Katika hatua nyingine, mwakani tutapokea Ripoti ya Tume ya Rais ya
Maboresho ya Kodi ambayo itatusaidia kuboresha wigo na mifumo ya kodi,
pamoja na kustawisha mazingira ya kibiashara nchini.
Katika
utekelezaji wa mapendezo ya Tume ya Haki Jinai, mwakani 2025
tutakamilisha Sera na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali
zinazohusiana na masuala ya haki jinai. Tutaendelea pia kutoa msaada wa
kisheria kwa wahitaji. Hadi sasa, jumla ya wananchi 495,552
wameshanufaika na Msaada wa Kisheria wa Kampeni ya Mama Samia Legal
Aid chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Ndugu zangu;
Mwaka 2025 ni mwaka maalum kwa maendeleo ya kisiasa na kidemokrasia
nchini. Tutafanya Uchaguzi Mkuu kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Wabunge na Madiwani, na kwa upande wa Zanzibar, tutachagua
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi na Madiwani. Miongoni mwa maandalizi ya awali ya
uchaguzi huo, ilikuwa ni kufanya mashauriano na wadau wote wa kisiasa
yaliyopelekea kurekebishwa kwa sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, na Sheria ya Vyama
vya Siasa. Ni imani yetu kwamba sheria hizo zitatuongoza vyema katika
kusimamia kwa ufanisi chaguzi zijazo. Nitoe rai kwa wananchi na wadau
wote wa uchaguzi kuhakikisha tunaidumisha sifa ya Nchi yetu ya kuwa na
demokrasia iliyojengeka juu ya msingi wa uhuru na haki.
Ndugu Wananchi;
Nilianza kwa kusema kuwa mwaka tunaoumaliza ulikuwa mwaka wa
kihistoria, wenye mafanikio na unaotupa matumaini zaidi kuhusu kesho ya
Taifa letu; na maelezo yangu yameonesha kwa nini nilisema hivyo.
Nikihitimisha, niseme tu kwamba, mwenendo mzuri wa uchumi, uwezo wa
kukabiliana na changamoto na kusimamia mipango yetu, na ari kubwa ya
wananchi kujiletea maendeleo, vinatupa sote matumaini makubwa sana
tunapoingia mwaka 2025. Nimalizie kwa kuwashukuru sana kwa imani na
ushirikiano mkubwa mliotoa kwa Serikali na kutuwezesha kutekeleza vyema
majukumu yetu. Nitoe shime kwa Watanzania kujenga ari na ujasiri wa
kufanya kazi kwa uadilifu, weledi, bidii na maarifa zaidi, katika
kuchangia maendeleo yetu.
Katika mwaka ujao 2025 na mengine
mingi ijayo, namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie afya njema na furaha
mioyoni mwetu. Tujaaliwe uwepo wa Amani na Utulivu nchini, kheri na
fanaka katika maisha yetu.
Mungu ibariki Afrika,
Mungu ibariki Tanzania,
Ahsanteni kwa kunisikiliza!
Nawatakia mwaka mpya wenye kheri.
Asante.
No comments:
Post a Comment