Dar
es Salaam. Tarehe 7 Januari 2025: Katika kuukaribisha mwaka mpya 2025,
Benki ya CRDB imezindua mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi
na sekondari nchini kote. Mikopo hiyo inayoitwa Ada Fasta ni mwendelezo
wa juhudi za Benki ya CRDB kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake
ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kifedha wanakokabiliana
nazo.
Akizindua mikopo hiyo inayotolewa kupitia Programu ya SimBanking, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo amesema kila mzazi au mlezi mwenye uhitaji anaweza kupata mkopo huo ili kumruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo kulingana na ratiba ya muhula husika.
“Mteja
anaweza kukopa mpaka shilingi milioni 3 ambazo atazirudisha ndani ya
miezi sita. Riba ya mkopo huu ni asilimia 13 tu mwaka, gharama ndogo
zaidi ukilinganisha riba iliyopo sokoni. Nawakaribisha wazazi wote
kuitumia fursa hii kuhakikisha watoto wetu wanasoma bila tatizo lolote
la ada,” amesema Nshekanabo.
Mkurugenzi
huyo amesema wameizindua huduma hiyo kipindi hiki wakitambua kuwa
Januari ni mwezi wenye changamoto nyingi za kifedha zinazotokana na
mahitaji makubwa yanayokuwepo ikiwamo ada za wanafunzi, kodi ya nyumba
na mahitaji mengine muhimu hasa baada ya kila mtu kuwa ametumia kiasi
kikubwa cha fedha kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Ikiwa
Benki inayomsikiliza mteja na kumweka mbele katika mikakati ya
biashara, amesema wakati wote wanabuni huduma na bidhaa zinazokidhi
mahitaji ya wateja na Januari hii wamekuja na jambo jipya mahususi kwa
kila mzazi au mlezi wa mwanafunzi nchini.
Zaidi
ya muongo mmoja Benki ya CRDB ilizindua nakuutambulisha Mfumo wa
Makusanyo ya Ada Shuleni yaani School Fees Management System ambao mpaka
sasa unatumiwa na zaidi ya shule 1,000 nchini kote ambazo sasa
wanafunzi wake watanufaika na mikopo hii iliyozinduliwa.
Mzazi
au mlezi atakayeomba mkopo huu, amesema atapata fedha husika
zitakazoingizwa kwenye akaunti ya shule moja kwa moja na yeye kupata
risiti ya uthibitisho kwamba amelipa ada inayotakiwa kwa ajili ya mtoto
wake.
Kwa kuwawezesha wazazi na walezi kulipa ada kwa wakati, Nshekanabo amesema wana imani watakuwa wamesaidia kuboresha elimu kwa kuwawezesha wanafunzi kuhudhuria masomo yao bila vikwazo huku shule zikiweza kujiendesha na kutoa maarifa bora yanayohitajika kwa watoto wa Kitanzania.
Kwa mzazi au mlezi ambaye ameajiriwa na mshahara wake unapitia Benki ya CRDB, anaweza kupata mkopo wa ada kwa kuingia kwenye Programu ya SimBanking kisha akabofya sehemu ya mikopo ambako atatakiwa kuingiza ‘control number’ aliyotumiwa na shule kwa ajili ya malipo ya ada na programu itamwonyesha kiasi cha juu anachoruhusiwa kukopa.
Baada
ya hapo, mteja atatakiwa kuingiza kiasi anachokitaka na kupendekeza
muda anaotaka kulipa deni hilo ndani ya miezi sita ili kukamilisha
maombi yake. Akishafanya hivyo, Benki ya CRDB itaingiza fedha
zilizoombwa kwenye akaunti ya shule anakosoma mtoto hivyo kumruhusu
asome kwa utulivu.
Ukiacha
faida zilizopo kwa pande zote mbili yaani shule na mzazi au mlezi,
mfumo wa makusanyo ya ada wa Benki ya CRDB ni rahisi kuutumia kwani
mteja anaweza kulipa ada kupitia SimBanking, CRDB Wakala au kutembelea
tawi la Benki ya CRDB.
Vilevile,
mteja anaweza kulipa ada ya mwanafunzi kupitia M-pesa, Tigopesa, Airtel
Money au Halopesa bila kulazimika kupeleka risiti ya malipo shuleni
kwani taarifa huwa zinafika huko moja kwa moja. Kwa upande wa shule,
faida iliyopo ni kwamba inakusanya ada kwa wakati na kupata taarifa papo
hapo.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kote (Ada Loan) iliyozinduliwa na Benki ya CRDB ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake kwa kuwawezesha mkopo ili kukabiliana na changamoto za kifedha hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka. Uzinduzi huo umefanyika leo kwenye ukumbi wa Benki hiyo, jijini Dar es salaam leo
No comments:
Post a Comment