Tuesday, January 07, 2025

MKUU WA WILAYA YA KINONDONI AVUTIWA NA MRADI WA SAMIA HOUSING SCHEME, KAWE

 

 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule akitembelea mradi wa Samia Housing Kawe wilayani Kinondoni muda mfupi baada ya kupewa maelezo ya mradi huo, pichani akisindikizwa na Meneja Miradi wa NHC, Mhandisi Grace Musita Wakurugenzi na Wahanddisi wengine katika mradi huo.

Samia Housing Kawe inavyoonekana sasa

 Mkuu wa Wilaya akikaribishwa na Msimamizi wa Mradi wa Kawe 711, QS Samuel Metili alipowasili kwenye mradi huo.

Mradi wa Kawe 711 ulivyo sasa.


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule akipata maelezo ya mradi wa Morocco Square kutoka kwa Msimamizi wa Mradi, Stanley Msofe.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule akipata maelezo ya mradi wa Morocco Square kutoka kwa Msimamizi wa Mradi, Stanley Msofe.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule  ameeleza kufurahishwa na maendeleo makubwa ya mradi wa kihistoria wa Samia Housing Scheme unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Kawe, jijini Dar es Salaam. 

Ziara yake ililenga kukagua hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo ambao ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha makazi kwa Watanzania.

Akiwa eneo la mradi, Mtambule alipokea taarifa kutoka kwa Injinia Grace Msita, ambaye alieleza kuwa mradi huo unalenga kujenga nyumba 5,000 kwa awamu. Alibainisha kuwa kazi zilizopo sasa ni kufunga milango, kuimarisha mifumo ya lifti, na kupanga njia za watembea kwa miguu (pavement). 

Mradi huu unakadiriwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 48 hadi kukamilika kwake, ambapo tayari kiasi cha shilingi bilioni 30 kimetumika kufanikisha hatua zilizofikiwa.

Aidha, akiwa katika mradi wa 711 Kawe, Mkuu wa Wilaya alikaribishwa na Msimamizi wa Mradi huo, QS Samuel Metili, ambaye alieleza kuwa kazi za ujenzi zimeendelea kwa kasi nzuri huku akibainisha ubora mkubwa wa kazi inayofanywa na Mkandarasi Esteem Construction. 

Mtambule alitoa pongezi kwa NHC kwa usimamizi bora wa miradi hiyo, akisema kuwa gharama nafuu zinazotumika ni ishara ya uwezo wa wataalamu wa ndani na pia ubora wa kiwango cha ju wa miradi ya 711 na Morocco Square ni ishara ya ubora wa mkandarasi na wasimamizi wake ambao ni NHC.

Alipotembelea mradi wa Morocco Square, Mkuu wa Wilaya alikaribishwa na Msimamizi wa Mradi, Stanley Msofe, ambaye alieleza kuwa majengo manne yaliyopo katika msingi mmoja yamepata mafanikio makubwa katika upangishaji. Kwa upande wa jengo la ofisi, upangishaji umefikia asilimia 100, wakati nafasi za biashara zimepangishwa kwa zaidi ya asilimia 90. Zaidi ya nyumba 76 kati ya 100 zilizopo katika mradi huo tayari zimeuzwa, huku utekelezaji wa ujenzi ukiwa umefikia asilimia 98.

Mtambule alisifu ufanisi wa NHC katika kusimamia miradi kwa ubora wa hali ya juu na gharama nafuu. "Iwapo mradi huu ungejengwa na mkandarasi wa nje, gharama zingefikia takriban shilingi bilioni 72. Hii ni ishara kwamba tunao wataalamu wa ndani wenye uwezo mkubwa," alisema. 

Aliongeza kuwa miradi hii inadhihirisha juhudi thabiti za Rais Samia katika kuleta maendeleo na kurejesha matumaini ya Watanzania kwenye miradi ya maendeleo.

Katika maelezo yake, Mtambule alitoa pongezi kwa Shirika la Nyumba la Taifa kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba zenye viwango bora na za kisasa ambazo si tu zinaongeza thamani ya Kinondoni, bali pia zinaboresha maisha ya wakazi. "Nyumba hizi ni uthibitisho wa dhamira ya Rais Samia ya kuboresha sekta ya makazi kwa vitendo. Tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu kwa kuona mbali na kuwekeza kwenye maendeleo ya watu," alisisitiza Mtambule.

Aidha, Mkuu wa Wilaya alihimiza NHC kuendeleza ubunifu na kupanua miradi kama huu hadi maeneo mengine kama Bunju, Madale, na Mabwepande, ambako kuna fursa nyingi za uwekezaji. "Tunapenda kuona makazi bora kama haya yanapatikana katika maeneo mengine, ili Watanzania wengi zaidi wanufaike na jitihada hizi," alisema.

Kwa upande wake, Shirika la Nyumba la Taifa liliwashukuru Mkuu wa Wilaya kwa ushirikiano na ushauri wake wa mara kwa mara. Shirika lilisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuboresha makazi na huduma kwa Watanzania, huku likitekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kumiliki au kuishi kwenye nyumba za kisasa kwa gharama nafuu.

Miradi ya Samia Housing Scheme, 711 Kawe, na Morocco Square si tu inaakisi ukuaji wa sekta ya ujenzi nchini, bali pia inachangia kukuza uchumi wa taifa na kuboresha mazingira ya maisha ya watu. Kupitia miradi hii, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuimarisha maisha ya wananchi na kuonyesha kuwa makazi bora ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania.

No comments:

Benki ya CRDB yaanza kutoa mikopo ya ada shule za msingi, sekondari

  Dar es Salaam. Tarehe 7 Januari 2025: Katika kuukaribisha mwaka mpya 2025, Benki ya CRDB imezindua mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule...