Sunday, January 12, 2025

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR AZINDUA TAWI LA NMB WETE, APOKEA VIFAA TIBA VYA MIL. 12

 








NA; MWANDISHI WETU, PEMBA

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Hemedi Suleiman Abdulla, amezindua Tawi la NMB Wete, lililopo Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, huku akiahidi kuwa SMZ itaendeleza ushirikiano wake na NMB, benki aliyoitaja kama kinara wa kusapoti jitihada za utekelezaji wa miradi mikubwa na ya kimkakati.

Uzinduzi wa NMB Tawi la Wete umefanyika Januari 10 na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, akiwemo Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) – Kanda ya Zanzibar, Ibrahim Malogoi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Zanzibar, Saada Mkuya Salum na Afisa Mkuu wa Fedha NMB, Juma Kimori.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Makamu wa Rais alisema tawi hilo ni muhimu sana kwa ustawi na maslahi mapana ya wananchi wa Kaskazini Pemba na Zanzibar kwa ujumla na kwamba mwitikio wa haraka wa wateja 1,800 waliofungua akaunti zao baada ya kufunguliwa unaakisi kiu ya maendeleo ya wakazi wa eneo hilo.

“Uzinduzi huu wa NMB Wete, ni jambo muhimu kwa maisha maslahi ya wananchi wa Kaskazini Pemba na Wazanzibar, Takwimu zimetolewa hapa kuwa siku chache kabla uzinduzi huu wateja 1,800 wamefungua akaunti, hii ni kuthibitisha kiu yao ya huduma zenu, ndio maana nasisitiza wananchi wachangamkie fursa.

“Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB ameeleza fursa nyingi na huduma nyingi watakazotoa hapa, nami nieleze kuwa wananchi karibieni tawini mjue huduma na fursa hizo na mzitumie, nasisitiza hilo huku nikiwaomba NMB waendelee kusambaza na kuboresha huduma zao kwa wananchi, hasa suala zima la huduma za kidijitali,” alisema Makamu wa Rais.

Aliongeza kuiwa SMZ Inaahidi ushirikiano mkubwa na NMB katika kufanikisha ustawi na maisha bora kwa Wazanzibar, akibainisha kuwa ubora wa kihuduma unaooneshwa na benki hiyo unatokana pia na mazingira mazuri na uwekezaji mzuri wa teknolojia uliofanywa.

“Ujio wa NMB Wete utaleta na kuchachua ushindani wa taasisi za fedha Kaskazini Pemba kihuduma, ambazo hazihitaji ushawishi wa maneno, bali huduma zenyewe ndio mshawishi mkuuu,” alisisitiza Abdullah huku akituma salamu za pongezi kwa Afisa Mtendaji Mkuu wake Ruth Zaipuna kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya.

“Kwa dhati kabisa shukrani zetu zimfikie CEO wa NMB, na salam zimfikie, tunamshukuru kwa ushirikiano wake na sapoti zake kwa SMZ n ahata Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hakika amekuwa mfano wa kuigwa, kazi kubwa anaifanya na tunampongeza kwa juhudi zake, utumishi na mashirikiano yake.

“Mambo mbalimbali yamesemwa jinsi waliyosaidia hapa Pemba, lakini ukiacha vifaa vya elimu na vifaa tiba vilivyotajwa, ipo ‘Ultra Sound’ moja haijatajwa, mliyotoa katika Hopsitali ya Kendwa ikiwa nma thamani ya zaidi ya Sh. Mil. 53, kupitia kifaa kile hospitali ile inafanya kazi kubwa kuliko hospitali ya wilaya,” alimalizia.

 Awali, Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu, Bi. Ruth Zaipuna, aliishukuru SMZ na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano bora inaoonesha kwa NMB na mazingira wezeshi inayoyaimarisha kila uchao katika kuziwezesha Taasisi za Fedha kuhudumia wananchi kwa ufanisi.

“Tuko hapa kuthibitisha kwa vitendo kaulimbiu yetu ya Karibu Yako, NMB Wete inaenda kumaliza adha ya wakazi wa hapa kusafiri umbali wa kilomita zaidi ya 30 kwenda Chakechake kufuata huduma za kibenki na sasa watapata huduma zote hapa tawini ikiwemo mikopo, kuweka na kutoa pesa, bima na kubadilisha fedha.

“NMB Wete ni tawi la 241 kote nchini Tanzania, likiwa ni tawi la tisa kwa Visiwani Zanzibar. Hii maana yake ni kwamba mtandao wetu wa huduma unaojumuisha ATM 720, kati ya hizo 22 zikiwemo hapa Zanzibar, unaendelea kukua kwa kasi na ahadi yetu ni kuzidi kusogeza huduma kwa Watanzania wote, kote nchini.

“Tunaahidi kuendelea kusafiri pamoja na serikali zote, hasa SMZ katika meli yake ya Uchumi wa Buluu, sera ambayo ni muhimu mno kwa ustawi wa Wazanzibari. Sambamba na uzinduzi huu, tunakabidhi vitanda 10 vya kulaza wagonjwa, vitano vya kujifungulia na mashuka 80 kwa Hospitali ya Mzambarauni, vyenye thamani ya Sh. Mil. 12.

“Vifaatiba hivyo tunavitoa kupitia fungu letu la Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambayo tunatumia asilimia moja ya faida yetu kurejesha kwa jamii kama tulivyofanya katika uezekaji wa mapaa ya Skuli ya Tasini na Kiwani tulikopaua shule na Kituo cha Afya Kendwa, ambako tumetumia zaidi ya Sh. Mil. 110,” alisema Kimori.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa BoT – Kanda ya Zanzibar, Ibrahim Joseph Malogoi, aliipongeza NMB kwa jitihada kubwa inazofanya katika kusambaza huduma za kibenki kwa jamii na kwamba NMB ni benki ya 14 Zanzibar na ya nne kufikisha huduma kwa Wananchi wa Pemba, huku Tawi la Wete likiwa ni tawi la 9 la benki.“

Kama msimamizi wa Serikali katika huduma za kibenki, nafarijika sana kuona ustawi wa Sekta ya Fedha Zanzibar ukikua kwa kasi na ongezeko hili la Taasisi za Fedha kwa Wazanzibar, linaakisi jitihada za dhati za kuimarisha ukuaji wa Uchumi na ndio maana halisi ya Mapinduzi,” alibainisha Malogoi.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Bi. Saada Mkuya Salum, aliipongeza NMB kwa kuzindua tawi jipya Wete, alioutaja kama muendelezo wa taasisi hiyo kusapoti Sera ya Ujumuishwaji wa Wananchi katika masuala ya fedha, ambayo kiwango cha Watanzania wanaotumia huduma hizo imeongezeka kwa kasi.

Alisema kupitia Shamrashamra za Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, miradi kadhaa mikubwa na ya kimkakati imezinduliwa, akisema imetokana na fedha ambazo Serikali imekopa kutoka kwa NMB na NBC, ambao kwa pamoja wameikopesha Sh. 470 na kwamba Ofisi ya Rais Fedha na Mipango inatambua na kuthamini mchango huo na inaahidi ushirikiano endelevu.

No comments:

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR AZINDUA TAWI LA NMB WETE, APOKEA VIFAA TIBA VYA MIL. 12

  NA; MWANDISHI WETU, PEMBA MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Hemedi Suleiman Abdulla, amezindua Taw...