BENKI ya NMB, imetangaza udhamini wa Sh. Milioni 50 wa michuano ya Kombe la Mapinduzi ya Zanzibar (Mapinduzi Cup 2025), inayotarajia kuanza Januari 03, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani visiwani Pemba, ambayo itashirikisha timu za Taifa, badala ya klabu za Tanzania Bara na Zanzibar kama ilivyozoeleka
Sambamba na udhamini huo, NMB pia imekabidhi
'tracksuit' 100 zenye thamani ya Sh. Mil. 9 za kuvaa viongozi wa
Serikali ya Zanzibar katika Siku ya Kitaifa ya Mazoezi (Januari 1,
2025), ambayo ni sehemu ya Shamrashamra za Miaka 61 ya Mapinduzi
Matukufu ya Zanzibar, ambayo inafanyika chini ya kaulimbiu: 'Amani,
Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo Yetu - Mapinduzi Daima.'
Hafla
ya makabidhiano ya hundi ya udhamini na 'tracksuit' hizo, imefanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Zanzibar, ambako Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Ahmed
Jumaa Nassor, alimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Fatma Hamad
Rajabu, mbele ya Meneja Uhusiano wa NMB Zanzibar, Jaha Khamisi.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo baada ya kupokea hundi, Bi. Fatma aliishukuru NMB
kwa mchango wao, ushirikiano na umoja wanaoonesha kwa Serikali ya
Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, na kuitaka
kudumisha mashirikiano hayo kwa ustawi wa Zanzibar na maendeleo ya
Wazanzibar kwa ujumla.
Alibainisha kuwa mchango na ushiriki wa
NMB sio tu katika Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, bali iko mstari wa
mbele daima kuchagiza maendeleo ya visiwa hivyo na wakazi wake na katika
nyanja nyingi, ikiwemo michezo, ambako imejitoa vya kutosha kudhamini
Kombe la Mapinduzi kwa miaka kadhaa na kuchangia ongezeko la ajira
kupitia michezo.
"Wazanzibar wengi wanahudumiwa na NMB na uwingi
wao unalenga kuiwezesha benki kukuza pato lao ili nao wanufaike na
mchango wa maendeleo ya Zanzibar na watu wake. Tunawapongeza kwa
kufadhili Siku ya Mazoezi Kitaifa, lakini pia kwa udhamini wenu mnono
katika Kombe la Mapinduzi 2025.
"Tofauti na miaka yote ambako
klabu hushiriki Kombe la Mapinduzi, mwaka huu zitacheza timu za Taifa,
ikiwemo Zanzibar Heroes. Wito wetu kama Serikali, tunawataka Wazanzibar
wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Gombani Pemba, kuisapoti timu yao iweze
kubakisha nyumbani taji la mashindano hayo," alisema Bi. Fatma.
Kwa
upande wake, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Ahmed Jumaa Nassor,
alisema benki yake inajisikia fahari kuwa sehemu ya Shamrashamra za
Mapinduzi ya Zanzibar kwa miaka 12 sasa na kwamba inatambua na
inathamini mchango wa Serikali ya Zanzibar katika kuweka mazingira
wezeshi ya wao kuhudumia Wazanzibar na kuunga mkono juhudi za maendeleo
ya wananchi.
"NMB imekuwa mshirika mkubwa wa Serikali zote
(Zanzibar na Tanzania), hivyo ni heshima kuendelea kuwa sehemu ya
Shamrashamra za Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
"Tuko
hapa kufanya mambo mawili, yote yakihusiana na sherehe hizo zinazoanza
Januari Mosi na kufikia ukomo wake Januari 13, siku moja baada ya kilele
cha Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
"Leo tunakukabidhi
'tracksuit' 100 za kuvaa washiriki wa Siku ya Mazoezi Kitaifa Zanzibar
Januari Mosi, tukiamini kuwa mchango huu utatumika kama chachu katika
muendelezo wa hamasa ya mazoezi miongoni mwa Wazanzibar, pia tunakabidhi
kwako hundi ya udhamini wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, wenye
thamani ya Sh. Milioni 50," alisema Ahmed na kuongeza:
"Udhamini
huu pamoja na vifaa hivi, ni kilelezo na uthibitisho wa dhati kuwa NMB
inathamini michezo, kwani afya zetu zinaimarika zaidi kupitia michezo na
uimara wa afya ndio chachu ya kukua kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na
Taifa kwa ujumla.
"Ni fahari kubwa kwetu kuendelea kushirikiana
na Serikali kwa miaka 12 ya NMB kuwa sehemu ya ukamilifu wa matukio hayo
kwa kipindi chote hicho," alisisitiza Ahmed katika hafla hiyo
iliyoshuhudiwa pia na maafisa wa wizara hiyo ya Habari, Vijana Utamaduni
na Michezo pamoja na Wajumbe wa kamati ya kombe la mapinduzi 2025.
No comments:
Post a Comment