Picha zote Kushoto ni Katibu Mkuu Joyce Mapunjo, Katikati Waziri Dkt Harrison Mwakyembe na Kulia ni Naibu Waziri Dkt Abdallah Juma Saadala. Huyo mwenye suti na tai nyekundu kwenye picha hizo mbili ni Naibu Katibu Mkuu Amantius Msole.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UAMUZI WA SERIKALI YA KENYA KUZUIA MAGARI YA KITALII YALIYOSAJILIWA TANZANIA KUINGIA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA JOMO KENYATTA KWA AJILI YA KUCHUKUA NA KUSHUSHA WATALII
Tarehe 22 Desemba, 2014, Serikali ya Jamhuri ya Kenya ilitoa amri ya kuzuia magari ya kitalii yenye usajili wa Tanzania kwenda kuchukua na kushusha watalii wanaotumia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta wakiwa njiani kuja kutembelea vivutio vya utalii katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Baada ya uamuzi huu wa Serikali ya Kenya, Waziri wa Maliasii na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu alifanya majadiliano na Waziri wa masuala ya utalii wa Serikali ya Kenya siku ya tarehe 16, Januari, 2015 ili kutafuta ufumbuzi wa kadhia hii. Matokeo ya mkutano wa Mawaziri hawa yalikuwa ni kusitishwa kwa muda katazo lililotolewa na Serikali ya Kenya kwa makubaliano kuwa yafanyike mazungumzo baina ya pande hizi mbili ndani ya kipindi cha wiki tatu kuanzia tarehe 16 Januari, 2015 ili kurekebisha Mkataba wa Ushirikiano katika sekta ya utalii wa mwaka 1985 kati ya nchi zetu mbili.
Kufuatia makubaliano hayo Wizara ya Maliasili na Utalii iliiomba Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki iandae kikao hicho cha pamoja katika muda uliopangwa. Kwa kuzingatia historia na uzito wa suala lenyewe, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki iliona umuhimu wa kuhusisha Wizara zingine husika za Uchukuzi, Mambo ya Nje, Viwanda na Biashara, Fedha, Ulinzi, Mambo ya Ndani, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na Viongozi wa Sekta Binafsi ili kupata msimamo wa nchi wa pamoja kabla ya mkutano na Kenya.
Hivyo, vikao vya wataalam vimefanyika Dar es Salaam na Arusha hadi wiki ya kwanza ya mwezi huu wa pili kwa maandalizi ya kikao cha mwisho cha Mawaziri upande wa Tanzania kabla ya kukutana na wenzetu wa Kenya. Pamoja na kushauriana na Waziri mhusika wa Kenya (Masuala ya Afrika Mashariki, Biashara na Utalii, Bi. Phyllis Kandie) kusogeza mbele tarehe ya mkutano wa pamoja ili kuruhusu muda wa kutosha kwa majadiliano ya ndani na wadau, Bi. Kandie alimwandikia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Dkt. Richard Sezibera na kumnakili Waziri Nyalandu, kurejesha amri yake ya awali ambayo alisema inaendana na Sheria ya utalii na kanuni za uchukuzi za Kenya.
Serikali ya Tanzania kimsingi imesikitishwa na uamuzi huo wa Serikali ya Kenya kwani haujengi wala hauendani na dhamira njema ya Mkataba wa Kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuenzi njia ya mazungumzo, maelewano na maridhiano katika kufikia maamuzi. Suala la kurekebisha mkataba ulioingiwa na nchi hizi mbili kwa hiari miaka 30 iliyopita, si jepesi la kujadiliwa na Mawaziri wawili tu na kuwekeana ukomo wa muda katika kulipitia. Serikali ya Tanzania itaendelea na mchakato iliouanzisha wa kuhusisha wadau wote na kufikia uamuzi ambao itauwasilisha kwa Serikali ya Kenya kupitia vikao rasmi vya Jumuiya.
Pamoja na kwamba amri hii ya Serikali ya Kenya inaenda nje ya mkataba wa 1985 kwa kuvihusisha hata viwanja vya ndege kuwa sehemu ya vivutio vya utalii, Serikali ya Tanzania itaheshimu na kuzingatia amri hiyo ili kulinda undugu na urafiki uliopo kati ya nchi zetu huku tukitafakari hatua za kuchukua ili kuondoa bughudha kubwa itakayotokea kwa watalii na wasafiri wetu wanaopitia uwanja huo wa Jomo Kenyatta. Aidha Tanzania itachukua hatua ya kuwafahamisha watalii na wageni wote wenye nia ya kutembelea vivutio vya kitalii vya Tanzania kutumia viwanja vingine vya ndege ili kuepuka kadhia na gharama zisizo za lazima.
Kwa upande wa Tanzania, viwanja vya ndege hasa vile vya Kimataifa vitaendelea kuwa sehemu ya malango ya kuingilia na kutokea kwenda kokote iwe ndani ya Jumuiya au nje ya Jumuiya na havitavichukuliwa kama vivutio vya utalii. Tanzania haitazuia magari ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au nchi nyingine yoyote kuingia katika viwanja vyake vya ndege kuleta au kuchukua watalii wanaopitia katika viwanja hivyo na kwenda katika nchi zao.
Mkataba wa mwaka 1985 kati ya Tanzania na Kenya ulilenga kutoa mwongozo wa ushirikiano katika Sekta ya Utalii kati ya nchi zetu mbili. Aidha, makubaliano hayo yalielekeza maeneo muafaka kwa ajili ya kubadilishana watalii huku ikizingatiwa kuondoa bugudha kwa watalii. Maeneo hayo ni pamoja na miji ya mipakani pamoja na miji rasmi iliyopendekezwa na kukubalika na pande zote mbili ikiwemo Nairobi ambako kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta kipo.
Mwisho, Tanzania itaendelea kuenzi undugu na urafiki uliojengeka kwa zaidi ya miaka 50 tokea uhuru kati ya nchi zetu mbili na suala dogo kama hili halitaweza kuteteresha uhusiano wetu mzuri.
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
10 FEBRUARI, 2015.
No comments:
Post a Comment