BUNGE Maalum la Katiba leo tarehe 9 Septemba, 2014 limeanza kazi yake ya kusoma na kujadili taarifa za Kamati mbalimbali zikiwemo Kamati namba Kumi na Mbili, Kamati namba Mbili, Kamati namba Moja, Kamati namba Nne, Kamati namba Nane, Kamati namba Tano, Kamati namba Tisa, Kamati namba Tatu, Kamati namba Sita pamoja na Kamati namba Kumi na Moja.
Baadhi ya mambo yaliyojadiliwa katika Bunge hilo ni pamoja suala la baadhi ya viongozi kumiliki akaunti zao za fedha nje ya nchi, haki za makundi mbalimbali nchini, haki za binadamu, masuala ya ndoa ya jinsia moja, haki za wafanyakazi na ajira, wajibu wa Waajiri nchini, haki za uzazi kwa wanawake, haki ya kuishi na sheria ya kunyonga, pia mambo yanayohusu Muundo wa Baraza la Usalama la Taifa.
Akizungumza wakati wa mjadala huo katika Bunge hilo, mjumbe wa Kamati namba Sita, Mhe. Charles Mwijage amesema kuwa si vema kwa viongozi nchini kujenga tabia ya kufungua akaunti na kuweka fedha zao nje ya nchi kwani kunakaribisha masuala ya wizi wa fedha toka ndani ya nchi kwenda nje ya nchi.
“Ni vema kiongozi yoyote anayetaka kumiliki fedha nje ya nchi aeleze ni wapi anamiliki hizo akaunti na nini anamiliki”, alisema Mhe. Mwijage.
Naye Mjumbe wa Kamati namba Tatu, Mhe. Nyambari Chacha Nyangwine amegusia kuhusiana na suala hilo akisema kuwa kuna haja ya kuwekwa kwa sheria itakayowabana viongozi wenye tabia ya kufungua akaunti za fedha nje ya nchi ili hali hiyo isiwepo nchini.
“Mambo ya kiongozi wa umma kumiliki akaunti ya fedha nje ya nchi si jambo jema, sheria izuie na ni vema kiongozi yoyote wa umma anayetaka kufanya hivyo basi afungue akaunti yake ndani ya nchi na sio vinginevyo”, alisema Nyangwine.
Mhe. Nyangwine pia amezungumzia kuhusu kuendelezwa kwa sekta ya viwanda nchini ili kuweza kujikwamua kiuchumi, hivyo ameisisitizia Serikali kuviendeleza viwanda vyake ili uchumi wa nchi uweze kukua na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Aidha, alliongeza kuhusu haki za wanaume huku akisema kuwa wanaume tayari wao wanazo haki zao tangu kuzaliwa kulingana na maandiko ya dini yanavyosema, hivyo ni vema sasa wanawake wakapewa kipaumbele kwa kupewa haki sawa yaani hamsini kwa hamsini.
No comments:
Post a Comment