Sunday, February 01, 2026

TANAPA YASHINDA TUZO YA MCHANGO BORA WA UTANGAZAJI UTALII TANZANIA BARA NA VISIWANI KATIKA TUZO ZA UBUNIFU SEKTA YA UMMA 2026









Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeibuka mshindi wa Tuzo ya Mchango Bora wa Ushirikiano katika kuendeleza utalii na kuitangaza Tanzania kama kivutio kimoja cha utalii kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, katika Tuzo za Ubunifu wa Sekta ya Umma 2026, hafla iliyofanyika jana Januari 31, 2026 katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar.

Tuzo hiyo ilitolewa na Bodi ya Tuzo za Ubunifu katika Sekta ya Umma kwa kutambua jitihada za TANAPA katika kushirikiana na Serikali ya Zanzibar pamoja na wadau mbalimbali kutangaza vivutio vya utalii, hasa vilivyopo katika ukanda wa pwani, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Saadani, Mikumi na Nyerere.

Aidha, tuzo hiyo ilipokelewa na Afisa Uhifadhi Mshitu Mshitu, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Ofisi Kiunganishi ya TANAPA visiwani Zanzibar, kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi CPA Musa Nassoro Kuji. Mshitu aliwashukuru waandaji wa tuzo hizo kwa kutambua mchango wa TANAPA kwa hasa katika nyanja ya kuitangaza nchi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Taasisi nyingine zilizotambuliwa katika hafla hiyo ni pamoja na Wizara ya Afya Zanzibar, ZHC, ZFDA, ZURA, ZAWEMA, ZAA, ZECO, ZPPRA, ZCT, ZIC, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar (CAG Zanzibar), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar (TAKWIMU Zanzibar), ZMA, ZIPA, ZVETA, IPA, ZAHRI, ZARI na ZBS, pamoja na taasisi nyingine nyingi za umma ambazo zimeonesha ubunifu, uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tuzo za Ubunifu wa Huduma za Umma (Public Sector Innovation Awards) Ndugu Steven Mkomwa, aliipongeza TANAPA kwa kuendelea kuwa miongoni mwa taasisi za umma zenye ubunifu baada ya TANAPA kuwa miongoni mwa taasisi zaidi ya 40 zilizopokea tuzo za ubunifu zilizopita zilizotolewa Desemba 16, 2025 Jijini Dar Es Salaam.

TANAPA imeendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), taasisi zote zilizopo chini ya Wizara, pamoja na wadau wote wa uhifadhi na utalii nchini, kuhakikisha kuwa Hifadhi za Taifa zinaendelea kutunzwa na kutangazwa ili kufikia malengo ya Serikali ya kuvutia watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030.

No comments:

Waziri Mkuu Asisitiza Umuhimu wa Maadili na Mshikamano Katika Jamii

  WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amehimiza malezi bora ya watoto na vijana kama silaha muhimu ya kudumisha maadili, mshikamano na amani k...