Wednesday, February 11, 2026

TAFITI ZATAJWA KUWA NGUZO MUHIMU KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO

 




Na WAF - Dar es Salaam

Imeelezwa kuwa tafiti ni nguzo kuu katika kuimarisha maandalizi na uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko nchini pamoja na kutoa ushahidi muhimu unaoongoza maamuzi ya sera, miongozo na mikakati ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, kusaidia ugunduzi wa mapema, ufuatiliaji wa magonjwa na uendelezaji wa vipimo, chanjo na tiba.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe leo Februari 11, 2026 wakati wa kikao na Taasisi ya Utafiti ya Jeshi la Marekani 'Walter Reed Army Institute of Research' (WRAIR) kilichofanyika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.

"Tanzania imeweka vipaumbele maalum vya kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na mwitikio wa magonjwa (IDSR), kutanua wigo wa uwezo wa maabara ikiwemo ufuatiliaji wa vinasaba, kuimarisha mifumo ya afya ya kidijitali na matumizi ya takwimu ili kufanya maamuzi," amesema Dkt. Magembe

Pia, ameelezea uwezo wa Hospitali ya Kibong'oto katika kufanya tafiti na Maabara ya Taifa katika kugundua na kufuatilia magonjwa ambapo Taasisi hizi zote zimepata ithibati ya Kimataifa.

Aidha, Dkt. Magembe amesema kuwa Serikali inaona fursa kubwa ya kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na Taasisi ya Utafiti ya Jeshi la Marekani ya Walter Reed (WRAIR), hususan katika kuimarisha mifumo ya tahadhari ya ugunduzi mapema wa Magonjwa ya milipuko, ufuatiliaji wake na uchambuzi wa takwimu, uhamishaji wa teknolojia na uimarishaji wa uwezo wa tafiti za ndani kupitia taasisi kama NIMR katika kudhibiti na kuwa na takwimu za usugu wa vimelea dhidi ya dawa (AMR).

Kwa upande wake Kanali Brianna Perata ambaye ni Kamanda wa Taasisi ya Utafiti wa Jeshi la Marekani ameahidi kuwa Taasisi hiyo ya Kijeshi ya Marekani itaendeleza ushirikiano na Tanzania hasa katika tafiti mbalimbali ili kuboresha sekta ya afya nchini na kuomba kuendelea kupewa ushiriliano na Tanzania.

Maeneo yaliyopendekezwa kwa ushirikiano wa haraka katika kikao hicho ni pamoja na kukusanya, kuunganisha na kuchambua takwimu za usugu wa vimelea dhidi ya dawa (AMR), kuimarisha uunganishaji wa takwimu za afya ya kidijitali na maabara katika mfumo mmoja wa kitaifa, kuimarisha uwezo wa maabara za kikanda hususan katika maeneo ya mipakani.

No comments:

RAS ARUSHA ASISITIZA UTENDAJI KAZI UNAOZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk. Toba Alnason Nguvila, amewasistiza watumishi wa Umma kufanya kazi kwa kufuata Sheria, taratibu na kanun...