Thursday, February 19, 2026

MSIPORE ARDHI ZA WANANCHI KWA KIGEZO CHA UWEKEZAJI-DKT. MWIGULU







Asema msimamo wa Rais Dkt. Samia ni maendeleo na uwekezaji

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wa Serikali wasipore ardhi za wananchi kwa kigezo cha uwekezaji kwani msimamo wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwa kinara katika maendeleo na uwekezaji

“Rais Dkt. Samia anasema watendaji Serikalini, kwenye maeneo ya mikoa, wilayani msipore ardhi za watu kwa kigezo cha uwekezaji au maendeleo. Kila mtu apewe haki yake, msitumie ubabe kupora maeneo ya watu; Naibu Waziri - TAMISEMI andikeni barua inayotoa maelekezo hayo,” amesema.

Amesema hayo leo (Alhamisi, Februari 19, 2026) wakati akizungumza na wakazi wa Mkuu, mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye jengo la utawala la Halmshauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa Rais Dkt. Samia anafanya kazi kubwa inayoleta heshima kwa Tanzania. “Kuna mambo yalikuwa yanaleta aibu kuyasema, lakini leo hii ndani ya kipindi cha miaka minne, Rais Dkt. Samia ameyatekeleza.”

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne, Rais Dkt. Samia amejenga majengo ya utawala katika halmashauri 143 ambazo hazikuwa na majengo yenye hali ya kuridhisha. “Pia amejenga hospitali 119 kwenye wilaya zote ambazo hazikuwa na hospitali za wilaya.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Kilimanjaro afuatilie tuhuma kwenye mradi wa mabwawa ya samaki uliopo eneo la Mraokeryo, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ambao umejengwa chini ya kiwango na kupunguza ukubwa wa bwawa lililotakiwa kujengwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Reuben Kwagiilwa amewaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuhakikisha kuwa kila mmoja anamsimamia aliye chini yake ili kuongeza uwajibikaji katika kutoa huduma kwa wananchi.

No comments:

BELEKO: TUKISHINDWA KUPANGA, TUNAPANGA KUSHINDWA

Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Masoko na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)...