Na Sixmund Begashe, Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watanzania wananufaika zaidi na rasilimali zao hivyo Wizara anayoiongoza itaendelea kushirikiana na wadau katika usimamizi wa urithi wa Maliasili na Utalii ili kufikia lengo hilo.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo jijini Dodoma kwenye kikao chake na wadau wa Uwindaji Wenyeji na Bucha za Nyamapori kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja wa sekta hizo muhimu kwa uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla.
Amebainisha kuwa, Serikali chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo bega kwa bega na wadau wa sekta binafsi hivyo uongozi wa Wizara hiyo hautakuwa na muhali kwa mtumishi yeyote atakaye kwamisha juhudi hizo za kuendelea kuwaletea watanzania tabasamu kwa kuwainua kiuchumi kupitia sekta ya Maliasili na Utalii.
Pamoja na kuwapongeza wadau hao kwa uzalendo wao, amewataka kuendelea kushikamana na Wizara hiyo ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na wa mtu mmoja mmoja ili kufungua fursa zaidi za uwekezaji na ajira hususani kwa vijana.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasi na Utalii anaeshughulika na Utalii, Bw. Nkoba Mabula, amewahakikishia wadau hao kuwa, ofisi yake itasimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Dkt. Kijaji ambayo yametokana na maono mbalimbali waliyotoa.







No comments:
Post a Comment