Na John Walter-Manyara
Wizara ya Maji imezindua mpango maalum wa uwekezaji katika maji safi, usafi wa mazingira na usafi binafsi wenye thamani ya shilingi bilioni 94.62, utakaotekelezwa wilayani Hanang’, mkoani Manyara.
Mpango huo wa miaka mitano unaotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la WaterAid Tanzania, umezinduliwa Februari 11, 2026 na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, katika hafla iliyofanyika wilayani humo.
Lengo kuu la mpango huo ni kutatua changamoto ya ukosefu wa maji katika vijiji vya wilaya ya Hanang’ na kuboresha huduma za usafi wa mazingira na usafi binafsi kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhandisi Mathew amesema kuwa rasilimali zinazotarajiwa kupatikana kupitia vyanzo vya kawaida hadi mwaka 2030 ni shilingi bilioni 41.75, hali inayoacha pengo kubwa la kifedha.
Kutokana na hali hiyo, amesisitiza umuhimu wa mchango kutoka sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo.
Naibu Waziri ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuziba pengo hilo kwa maslahi ya wananchi, na kuhakikisha mpango huo unaingizwa kikamilifu katika mipango na bajeti za kila mwaka.
Pia amewahimiza wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuuona mpango huo kama ramani na mwaliko rasmi wa kuwekeza katika Wilaya ya Hanang’.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Almish Hazal, amemshukuru Naibu Waziri kwa jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau katika kuimarisha miradi ya maji.
Hata hivyo, ameeleza kuwa changamoto kubwa inayokabili miradi ya visima ni upatikanaji wa nishati, hususan majenereta, akibainisha kuwa matumizi ya sola bado ni tatizo kutokana na hali ya baridi katika wilaya hiyo.
Ameomba kuwepo kwa ushirikiano kati ya Tanesco na RUWASA ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika miradi ya maji, hatua itakayosaidia “kumtua mama ndoo kichwani kwa asilimia 100.”
Naye Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, huku akiiomba kutoa kipaumbele katika rasilimali zitakazohitajika wakati wa utekelezaji wa mpango huo.
“Leo hii tunapouweka mpango huu mezani, tunatoa mwaliko wa wazi kwa kila mmoja kushiriki. Tunaishukuru Serikali kwa ushirikiano wake, lakini tunaomba iendelee kuongoza kwa kutoa kipaumbele katika uwekezaji wa mpango huu, Washirika wa maendeleo na sekta binafsi waweke nguvu zao pale ambapo mpango wa Serikali unaelekeza,” amesema Mzinga.
Uzinduzi wa mpango huo unatarajiwa kuwa chachu ya maboresho makubwa ya huduma za maji na usafi wa mazingira katika Wilaya ya Hanang’, na kuchangia ustawi wa afya na maendeleo ya wananchi wake.




No comments:
Post a Comment