Saturday, February 14, 2026

KAKAMA Yatimiza Miaka 10: Serikali Zasisitiza Ushirikiano wa Kikanda Kukuza Kiswahili Afrika Mashariki



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na viongozi mbali mbali na wadau wa lugha ya kiswahili katika Maadhimisho ya kutimia miaka kumi (10) ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.


Serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeendelea kutambua na kuthamini mchango wa Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) katika kukuza, kuratibu na kuendeleza matumizi ya Kiswahili kama chombo cha mawasiliano na maendeleo ya kikanda.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, katika Maadhimisho ya Miaka 10 ya KAKAMA yaliyofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar Airport, Zanzibar.

Amesema katika kipindi cha muongo mmoja, KAKAMA imechukua hatua mahsusi za kuhakikisha wanajumuiya wa Afrika Mashariki wanatumia Kiswahili katika mawasiliano ya kila siku, hatua ambayo imechangia kukua kwa kasi kwa lugha hiyo na kuimarisha mshikamano wa kikanda. Ameeleza kuwa kwa kuzingatia ukubwa na ushawishi wa Kiswahili barani Afrika na duniani, ni wajibu wa Kamisheni kuhamasisha nchi wanachama kuanzisha na kuimarisha mabaraza ya kitaifa yatakayoratibu matumizi na maendeleo ya Kiswahili kwa mtazamo wa kimkakati.

Makamu huyo wa Pili wa Rais amegusia pia hatua ya UNESCO kuitambua Kiswahili kama moja ya lugha za kazi katika taasisi hiyo ya kimataifa, akisema uamuzi huo umefungua dirisha jipya la fursa kwa wataalamu wa Kiswahili katika nyanja za elimu, tafsiri, tafiti na diplomasia ya utamaduni. Ameitaka KAKAMA kujipanga kitaasisi ili kunufaika ipasavyo na fursa hizo kwa manufaa ya wanachama wote.

Ameihakikishia Kamisheni kuwa Serikali zitaendelea kutoa ushirikiano wa kisera, kifedha na kitaalamu ili kuhakikisha Kiswahili kinakuwa chombo madhubuti cha kufanikisha maendeleo endelevu ndani ya Jumuiya.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mheshimiwa Riziki Pembe Juma, ameipongeza KAKAMA kwa mafanikio ya miaka kumi, akieleza kuwa Kamisheni imepanua wigo wa matumizi ya Kiswahili katika sekta za elimu, biashara na mawasiliano ya kikanda na kimataifa. Amesisitiza kuwa Kiswahili si tu urithi wa utamaduni, bali ni rasilimali ya kiuchumi na kiutambulisho kwa mataifa ya Afrika Mashariki.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mheshimiwa Beatrice Askul Moe, amesema kuanzishwa kwa KAKAMA ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya kuziunganisha nchi wanachama kupitia lugha moja ya mawasiliano. Amehimiza nchi ambazo bado hazijaanzisha mabaraza ya kitaifa ya Kiswahili kufanya hivyo kwa haraka ili kuimarisha uratibu na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa sera za lugha katika ngazi ya taifa na kikanda.

Akitoa salamu za mabaraza na wadau wa Kiswahili, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Bi. Consolata Mushi, amesema katika kipindi cha muongo mmoja, KAKAMA imefanikiwa kuipa Kiswahili hadhi pana zaidi na kukifanya kuwa lugha rasmi ya mawasiliano, elimu na biashara katika eneo la Afrika Mashariki, huku ikiendelea kupenya katika majukwaa ya kimataifa.

Maadhimisho ya miaka 10 ya KAKAMA yameibua mjadala mpana juu ya nafasi ya Kiswahili kama nyenzo ya diplomasia ya utamaduni, uchumi wa maarifa na chachu ya ujumuishaji wa kikanda, yakionesha kuwa mustakabali wa lugha hiyo unategemea mshikamano wa kisera, uwekezaji wa kimkakati na ubunifu endelevu.

#KiswahiliMiaka10 #KAKAMA  #UmojaWaAfrikaMashariki #LughaNaMaendeleo  #DiplomasiaYaUtamaduni

No comments:

RAIS SAMIA AONGOZA MJADALA WA MAJI NA MAENDELEO AFRIKA, AKUTANA NA WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA ADDIS ABABA

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendeleza diplomasia ya kimkakati kwa kushiriki Mkutano wa...