Sunday, February 01, 2026

WAZIRI MCHENGERWA AONGOZA MAZOEZI KM 4.6 DHIDI YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

 


Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, leo Februari Mosi ameongoza mazoezi ya kutembea umbali wa kilomita 4.6 kuanzia Uwanja wa Benjamin Mkapa hadi Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi ya mwili kwa lengo la kuimarisha afya.

Mhe. Mchengerwa amesema kuwa mazoezi ya mwili ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na figo, ambayo yamekuwa yakiongezeka nchini na kusababisha gharama kubwa za matibabu kwa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuhimiza Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kula lishe bora na kuepuka tabia hatarishi ili kujenga jamii yenye afya na tija katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, mazoezi ya mwili huchangia kuboresha afya ya moyo na mishipa ya damu, kuimarisha misuli na mifupa, pamoja na kupunguza hatari ya udhaifu wa mwili unaosababishwa na kutofanya shughuli za kimwili.

Aidha, amesema mazoezi husaidia kuboresha afya ya akili kwa kupunguza msongo wa mawazo na sonona, kuongeza umakini na ufanisi kazini, pamoja na kudhibiti uzito wa mwili na unene uliopitiliza.

Waziri Mchengerwa amewataka wananchi, taasisi na waajiri nchini kuanzisha na kuendeleza programu za mazoezi ya mwili katika maeneo ya kazi na makazi ili kukuza mtindo bora wa maisha na kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa.

Mazoezi hayo yamehudhuriwa na watendaji mbalimbali wa Wizara ya Afya, wadau wa sekta ya afya pamoja na wananchi wa jijini Dar es Salaam, walioungana na Waziri katika kuonyesha kwa vitendo umuhimu wa kufanya mazoezi kama sehemu ya maisha ya kila siku

No comments:

Waziri Mkuu Asisitiza Umuhimu wa Maadili na Mshikamano Katika Jamii

  WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amehimiza malezi bora ya watoto na vijana kama silaha muhimu ya kudumisha maadili, mshikamano na amani k...