Sunday, February 01, 2026

ULEGA AAGIZA MKATABA WA MKANDARASI MCHINA UVUNJWE


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza kuanza utaratibu wa kuvunja mkataba wa kampuni ya ujenzi kutoka China ambayo imekuwa ikisuasua katika ujenzi wa barabara ya Omurushaka – Kyerwa mkoani Kagera yenye urefu wa kilomita 50.

Pamoja na agizo hilo, Waziri Ulega pia amezitaka mamlaka zinazohusika na utoaji wa kazi za ujenzi wa barabara kuiweka kampuni hiyo, Shandong Luquiao Group, katika orodha ya kampuni zisizotakiwa kupewa kazi za ujenzi wa barabara hapa nchini kwa sababu rekodi yake kwa kazi ilizopewa hairidhishi. 

"Natoa maelekezo kwa TANROADS na Mkurugenzi wa Barabara kutoka wizarani mpitie taratibu za kuvunja mkataba kwa mkandarasi huyu ndani ya mwezi mmoja ili tuweze kumchukulia hatua za kisheria, hatuwezi kuona fedha za wananchi zinachezewa kwa namna hii", amesema Ulega

Waziri Ulega ametoa maelekezo hayo katika mkutano na wananchi wa Kyerwa mara baada ya kumaliza ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.

Katika mkutano huo, Waziri Ulega alitoa maagizo kwa wataalamu wa sheria kuwa wanatakiwa kufuata vigezo vyote vya kisheria ili baadaye serikali isiingie katika kesi ambazo zitaigharimu fedha nyingi kwa sababu ya kushauriwa vibaya na wataalamu. 

Awali katika taarifa zao kwa waziri , Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa na Mbunge wa Kyerwa, Khalid Nsekela, walieleza kutofurahishwa kwao na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na ukweli kwamba pamoja na rekodi ya kusuasua kwake, mkandarasi huyo ameendelea kupewa kazi za ujenzi mkoani humo.

Kwa mujibu wa taarifa ya TANROADS, mkandarasi huyo tayari amelipwa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni tisa na ingawa alitakiwa kuwa amefikia walau asilimia 50 ya lengo, hadi sasa yuko katika asilimia tano tu ya utekelezaji wa mradi.

Katika hotuba yake hiyo, Ulega aliitaka TANROADS kutafuta suluhisho la haraka kwa kumtafuta mkandarasi wa ndani mwenye uwezo atakayeikarabati barabara hiyo ndani ya mwezi mmoja ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.

Ametoa rai kwa wasimamizi wa miradi kutoka TANROADS kuhakikisha wanasimamia vyema miradi kwa mujibu wa mkataba ambapo amesema pia wasimamizi wa mradi huo wachunguzwe endapo kama wamehusika kwenye uzembe wa ucheleweshaji wa mradi huo ili hatua zichukuliwe pia dhidi yao.

Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwasa amesema mkandarasi huyo amekuwa akisuasua pia katika utekelezaji wa miradi mingine ikiwemo ya TARURA katika mkoa huo na kushauri serikali kusitisha mikataba hiyo na kutompa zabuni tena mkandarasi huyo.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Ulega, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Kagera, Eng. Joel Mwambungu, amesema kuwa mradi huo kwa sasa umefika asilimia 5.43 na unafadhiliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 94.

Ameongeza kuwa mradi huo upo nyuma kwa asilimia 46.26 ambapo ni tofauti kati ya maendeleo yaliyotarajiwa ya asilimia 51.69 huku maendeleo halisi yaliyofikiwa yakiwa asilimia 5.43 pekee.









No comments:

Waziri Mkuu Asisitiza Umuhimu wa Maadili na Mshikamano Katika Jamii

  WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amehimiza malezi bora ya watoto na vijana kama silaha muhimu ya kudumisha maadili, mshikamano na amani k...