Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza katika Baraza Kuu la Wafanyakazi la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati wa kikao chake cha siku mbili mkoani Arusha tarehe 11 Februari 2026.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika hilo Bw. Hamad Abdallah akizungumza katika kikao cha Baraza jijini Arusha tarehe 11 Februari 2026.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja ya Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na baadhi ya wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wakati wa Kikao kilichofanyika tarehe 11 Februari 2026 jijini Arusha. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amewasisitiza wananchi wenye maeneo ya ardhi, kuhakikisha wanayaendeleza kabla serikali haijaanza kuchukua hatua.
Dkt. Akwilapo ametoa kauli hiyo leo tarehe 11 Februari 2026 wakati akifungua Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kinachoendelea jijini Arusha.
Akwilapo amesema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wananchi kununua maeneo ya ardhi na kuyahifadhi kwa muda mrefu kama mtaji kwa lengo la kupata faida baadaye.
“Bado natafakari nifanye nini maana sheria ipo, usipoendeleza eneo lako ndani ya miaka mitatu unaweza kunyang’anywa na wengi wanafanya ardhi kama mtaji. Nadhani kuna taasisi maalum za kukuza mitaji, kama vile Soko la Hisa la Dar es Salaa na UTT-AMIS, tumieni hizo taasisi. Huku ardhi tutapishana maneno”. Amesema Dkt Akwilapo.
Sheria ya Ardhi Sura Namba 113 kifungu cha 49 inaeleza wazi kuwa mmiliki wa ardhi asiyeendeleza eneo lake katika kipindi cha miaka mitatu serikali inaweza kulichukua eneo lake kutokana na kushindwa kuliendeleza.
Kupitia kikao hicho cha Baraza la wafanyakazi, Mhe. Dkt Akwilapo amewataka waendelezaji milki nchini likiwemo Shirika la Nyumba la Taifa, kuhakikisha wananchi wanapata nyumba bora na za gharama nafuu ili watanzania waweze kuwa na tabasamu.
Amewaasa watumishi wa NHC kuzingatia utu, maadili, uwazi na uaminifu wakati wote wa kutekeleza majukumu yao huku wakiachana na ile dhana ya kuuliza watapata kitu gani ndani ya shirika na badala yake wajiulize watalifanyia nini shirika hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi la NHC ambaye pia ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Bw. Hamad Abdallah amesema shirika lake limekuwa likifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha linaboresha maslahi ya watumishi.
Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi cha Shirika la Nyumba la Taifa kilichoanza leo tarehe 11 Februari 2026 kinatarajiwa kuhitimishwa Alhamisi tarehe 12 Februari 2026. Kikao hicho pamoja na mambo mengine kinajadili Mizania na Bajeti ya NHC kwa mwaka wa fedha 2026/2027.







No comments:
Post a Comment