Tuesday, February 03, 2026

RAIS SAMIA AANZA ZIARA YA KIKAZI DUBAI, AONGEZA KASI YA DIPLOMASIA YA KIUCHUMI NA UWEKEZAJI


Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameanza rasmi ziara ya kikazi nchini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), akilenga kuimarisha diplomasia ya kiuchumi, kupanua wigo wa ushirikiano wa kimataifa na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja nchini Tanzania.

Katika ratiba ya leo, Rais Samia anafanya mazungumzo ya ngazi ya juu na Mheshimiwa Gaston Browne, Waziri Mkuu wa Antigua and Barbuda, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi rafiki. 

Aidha, Rais Samia anakutana na Bi. Shaikha Al Nuwais, Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism), kwa mazungumzo ya pande mbili yanayolenga kuendeleza sekta ya utalii kama nguzo muhimu ya uchumi na kichocheo cha uwekezaji.

Jioni ya leo, Rais Samia anatarajiwa kushiriki uzinduzi wa Global Africa Investment Summit (GAIS), jukwaa mahsusi la uwekezaji linalolenga kuoanisha miradi iliyo tayari kuwekezeka barani Afrika na wawekezaji wa kimataifa. Ushiriki wa Tanzania katika GAIS unaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kugeuza fursa kuwa matokeo halisi ya kiuchumi.

GAIS ni mpango wa kimkakati unaoendeshwa sambamba na majadiliano ya sera ya World Governments Summit (WGS), ukiwa na lengo la kubadili mijadala ya sera kuwa uwekezaji wenye tija, unaochochea ukuaji wa uchumi, ajira na maendeleo endelevu barani Afrika.

Wananchi wanaendelea kushauriwa kufuatilia taarifa zaidi kupitia akaunti rasmi za Ikulu Mawasiliano, kwa maendeleo ya ziara hii muhimu kwa mustakabali wa uchumi wa Taifa.

No comments:

DKT. MWIGULU AKUTANA NA NAIBU MKURUGENZI WA FAO

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amefanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Bi...