Sunday, February 01, 2026

Waziri Mkuu Asisitiza Umuhimu wa Maadili na Mshikamano Katika Jamii

 


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amehimiza malezi bora ya watoto na vijana kama silaha muhimu ya kudumisha maadili, mshikamano na amani katika jamii, huku akitahadharisha dhidi ya wanaoingilia masuala ya imani, hatua ambayo inaweza kuhatarisha mshikamano wa Taifa.

Akizungumza leo jumapili Februari 01, 2026 katika ibada ya Kanisa Kuu la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Arusha Mjini, iliyokuwa ikiongozwa na Baba Askofu Dkt. Godson Abel Mollel, Waziri Mkuu alisema mmomonyoko wa maadili unaoanza na kejeli mitandaoni, dharau kwa wazee na viongozi pamoja na kukosa staha kwa mamlaka, unaweza kuathiri misingi ya Taifa endapo hautadhibitiwa mapema kupitia malezi thabiti.





Waziri Mkuu pia alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za dini, ikiwemo kurekebisha sheria ili taasisi za dini zisichukuliwe kama taasisi za kibiashara, kuweka mifumo ya misamaha ya kodi, na kutatua changamoto za akaunti zilizokuwa zimefungwa kutokana na masuala ya kikodi.

Katika Ibada hiyo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu alisema kuwa Rais Samia ametoa kiasi cha shilingi milioni 50 ili kuunga mkono juhudi za Ujenzi wa Kanisa Kuu la KKKT Arusha ambalo ujenzi wake ulianza Januari 2021.

Kanisa hilo jipya litakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 1,000, parking ya magari 200, ofisi, madarasa, chumba cha kunyonyeshea watoto, Chumba cha Mawasiliano na Teknolojia, na madhabahu inayoning’inia.

Waziri Mkuu aliwataka Watanzania kuendelea kujenga Taifa lenye heshima, maadili na mshikamano, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila misingi imara ya malezi na utu.

Awali, Baba Askofu Dkt. Godson Abel Mollel alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti wa Taifa na aliwahimiza waumini, hususan vijana, kutulia, kuepuka vurugu, na kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake.

No comments:

Waziri Mkuu Asisitiza Umuhimu wa Maadili na Mshikamano Katika Jamii

  WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amehimiza malezi bora ya watoto na vijana kama silaha muhimu ya kudumisha maadili, mshikamano na amani k...