Sunday, February 01, 2026

DKT. MSEMWA: UTEKELEZAJI WA DIRA 2050 KUANZA JULAI 1, 2026

 





Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Dkt. Fred Msemwa, amesema kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 utaanza rasmi Julai 1, 2026 ukiwa na lengo la kuhakikisha ustawi wa kila Mtanzania bila kujali hali yake.

Aidha amebainisha kuwa dira hiyo inalenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa na ushiriki wa wananchi wote katika maendeleo ya Taifa huku ikisisitiza kutomuacha nyuma Mtanzania yeyote.

Dkt. Msemwa ameyabainisha hayo Februari 01, 2026 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua za maandalizi ya kuanza kwa utekelezaji wa Dira 2050.

Amesema kuwa Dira 2050 ilizinduliwa Julai 17, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na baadaye Serikali kuielekeza NPC kuandaa mipango ya utekelezaji wake ikiwemo Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa Miaka 25 (2026/2027–2050/2051), Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/2027–2030/2031) pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027.

Aidha amebainisha kuwa mipango hiyo imepitia mashauriano ya kitaalamu na inatarajiwa kuwasilishwa Bungeni Februari 2, 2026 kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Amesema kuwa NPC imezingatia uzoefu wa utekelezaji wa Dira ya 2025 na ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miradi ya Taifa (NPMIS) utakaotumika kufuatilia utekelezaji wa Dira 2050 kuanzia Julai 2026 huku wananchi na wadau wakihimizwa kufuatilia mchakato huo kwa karibu.

No comments:

Waziri Mkuu Asisitiza Umuhimu wa Maadili na Mshikamano Katika Jamii

  WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amehimiza malezi bora ya watoto na vijana kama silaha muhimu ya kudumisha maadili, mshikamano na amani k...