Wednesday, February 11, 2026

WAZIRI WA ARDHI AIELEKEZA NHC KUPUNGUZA GHARAMA ZA UJENZI NA KUIMARISHA NIDHAMU YA MAPATO

Mgeni rasmi katika kikao hicho, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt. Leonard Akwilapo akifungua rasmi kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHC kwenye hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha leo.
Katibu Mkuu wa Chama cha wafanyakazi wa migodi, nishati, ujenzi na kazi nyingine -TAMICO Taifa, Bw. Partenus P. Rwechungura, akiwasilisha hoja za Tamico Taifa kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah na Mwenyekiti wa Kikao cha Baraza akitoa maelezo ya Utangulizia kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua rasmi kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHc kwenye hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha leo.
Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala, Fatuma Chilo akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo na baadaye Kumkaribisha Mwenyekiti. wa Baraza.
Katibu wa Chama cha wafanyakazi wa migodi, nishati, ujenzi na kazi nyingine -TAMICO NHC, Rebecca Lukule akitoa maelezo kwenye mkutano huo kabla ya mgeni rasmi hajafungua mkutano huo.
Mgeni rasmi katika kikao hicho, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt. Leonard Akwilapo akikabidhi cheti na tuzo kwa Mfanyakazi bora wa NHC Hindu Mwema baada ya kufungua rasmi kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHC kwenye hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha leo.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kudhihirisha dhamira ya kujenga mahusiano imara kati ya menejimenti na wafanyakazi, kufuatia kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilicholenga kuimarisha ustawi wa watumishi na kuongeza tija ya Shirika.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa TAMICO Taifa, Bw. Partenus Rwechungura, alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa NHC. Hamad Abdallah kwa kuliongoza Shirika kwa ufanisi huku akizingatia maslahi ya wafanyakazi. 

Alieleza kuwa uongozi thabiti na unaojali ustawi wa watumishi ni msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote ya umma.

Bw. Rwechungura alipendekeza kufanyika kwa maboresho ya Mkataba wa Hali Bora wa NHC uliopo, kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa haki, stahiki na maslahi ya wafanyakazi. Alibainisha kuwa hatua ya Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, kutoa muda wa miezi sita kwa ajili ya maboresho ya mkataba huo ni ya msingi na inaonesha utayari wa pande zote kujenga makubaliano yenye manufaa ya pamoja.

Alisisitiza kuwa marejeo ya mkataba yanapaswa kuzingatia maboresho ya stahiki mbalimbali ikiwemo posho za makazi (house allowance) na masuala mengine yanayogusa ustawi wa watumishi, ili kuhakikisha mazingira bora ya kazi na motisha endelevu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Hamad Abdallah, alimpongeza Bw. Rwechungura kwa kuendelea kusimama kidete kutetea maslahi ya wafanyakazi na kuhimiza mazungumzo yenye tija kati ya menejimenti na watumishi.

Abdallah amesema mtaji wa Shirika umefikia shilingi trilioni 6.9, hatua inayodhihirisha uimara wa taasisi hiyo na kuongezeka kwa thamani ya vitega uchumi vyake nchini. Amesisitiza kuwa ukuaji huo unatokana na usimamizi madhubuti wa miradi, ubunifu katika uendelezaji wa majengo ya biashara na makazi, pamoja na kuimarika kwa mikakati ya ukusanyaji mapato.

Mgeni rasmi katika kikao hicho, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt. Leonard Akwilapo, alilipongeza Shirika kwa utendaji mzuri uliowezesha kupata faida ya shilingi bilioni 58.86. Alieleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano kati ya uongozi na wafanyakazi, na kwamba ni muhimu mshikamano huo ukaendelezwa.

Dkt. Akwilapo aliwahimiza wafanyakazi kuwa na subira katika kipindi cha miezi sita kilichotengwa kwa ajili ya maboresho ya Mkataba wa Hali Bora, akisisitiza kuwa taratibu za kisheria na kiutawala lazima ziheshimiwe kabla ya mkataba kuwasilishwa na kuidhinishwa na mamlaka husika.

Aidha, alikumbusha kuwa NHC ina wajibu mkubwa kwa Watanzania wa kuwapatia makazi bora na yenye gharama nafuu, jambo ambalo ni kipaumbele cha Shirika. Katika kufanikisha hilo, aliielekeza NHC kuongeza jitihada za kupunguza gharama za ujenzi, hususan kwa kutafuta na kupata vifaa vya ujenzi kwa bei nafuu, hatua itakayowezesha nyumba kuuzwa kwa wananchi kwa gharama himilivu.

Waziri Akwilapo pia alieleza kuwa Wizara ipo tayari kushirikiana na NHC kwa kuwezesha uratibu na taasisi nyingine ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika.

 Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya mapato, kukusanya kodi na kudai madeni kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo, ili kuhakikisha uendelevu wa kifedha wa Shirika.

Katika kuimarisha utendaji, alihimiza kukamilishwa kwa miradi kwa wakati ili kupunguza uhaba wa makazi nchini, pamoja na kuimarisha mifumo ya ndani ya usimamizi wa fedha ili kupunguza mianya ya upotevu wa mapato.

 Alisisitiza pia kuimarishwa kwa utawala bora, kuondoa rushwa na uzembe, na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ikiwemo uwazi na uadilifu.

Kwa ujumla, kikao hicho kinachoendelea kesho kimeonesha dhamira ya pamoja ya kujenga Shirika lenye mshikamano, linalothamini rasilimali watu wake na kutekeleza wajibu wake kwa jamii kwa ufanisi. 

Mahusiano chanya kati ya waajiri na waajiriwa yameendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya NHC ya kutoa makazi bora na ya gharama nafuu kwa Watanzania.

No comments:

RAS ARUSHA ASISITIZA UTENDAJI KAZI UNAOZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk. Toba Alnason Nguvila, amewasistiza watumishi wa Umma kufanya kazi kwa kufuata Sheria, taratibu na kanun...