Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema jukumu la msingi la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kuhakikisha inalinda wananchi na mali zao pamoja na kutenda haki kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Hemed ameyasema hayo alipokutana na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi uliofika Ofisini kwake katika Baraza la Wawakilishi, Chukwani, Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha rasmi.
Amesema usalama wa raia na mali zao ni nguzo muhimu katika kuimarisha shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Amefafanua kuwa bila uwepo wa amani na utulivu, jitihada za maendeleo haziwezi kuzaa matunda yanayotarajiwa. Hivyo, Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vina wajibu wa kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu wakati wote.
Makamu wa Pili wa Rais amesisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu ya vyombo vya ulinzi na usalama unapaswa kuzingatia Katiba, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ili kuimarisha utawala bora na kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi za dola. Aidha, amehimiza matumizi ya teknolojia katika utendaji wa kazi za kila siku ili kuongeza ufanisi, uwazi na kasi ya utoaji huduma.
Sambamba na hilo, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano na miongozo stahiki kwa Wizara hiyo ili kuhakikisha inatekeleza kikamilifu maagizo ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Pascal Katambi (Mb), amesema dhamana waliyopewa ya kulinda usalama wa wananchi na mali zao ni kubwa na ya heshima. Ameahidi kuwa Wizara hiyo itaendelea kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na kwa kuzingatia misingi ya Kikatiba, Kisheria, taratibu, kanuni na miongozo ya nchi.
Waziri Katambi amesema watumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii na nidhamu, kwa kulinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuimarisha Muungano na kuzilinda tunu za Taifa ili kuendelea kuipa Tanzania heshima ndani na nje ya mipaka yake.
Ameongeza kwa kuwapongeza viongozi wakuu wa nchi kwa kuliongoza Taifa kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, utawala wa sheria, haki za binadamu na ustawi wa wananchi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Katika ziara hiyo, Mhe. Katambi aliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, Katibu Mkuu Ndugu Ally Senga Gugu, pamoja na Mkurugenzi wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Ndugu Miriyam Pereele Mmbanga.



No comments:
Post a Comment