Katibu wa CCJ, Renatus Muabhi (mwenye shati la kijani) na Mwenyekiti Richard Kiyabo (mwenye shati la cream).
SIKU nne baada ya Msajili wa vyama vya Siasa John Tendwa kutoa usajili wa muda kwa Çhama Cha Jamii (CCJ) kinachohusishwa na vigogo wa CCM, chama hicho kimesema kitasimamisha mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mwenyekiti wa muda wa chama hicho, Richard Kiyabo aliliambia Mwananchi Jumapili katika mahojiano maalum kuwa jana kuwa kuwa na mgombea wa urais katika uchaguzi huo ndilo lengo lao la msingi kusajili chama hicho sasa.
Alisema mbali na kumsimamisha mgombea urais, CCJ inajipanga kusimamisha wagombea wa ubunge katika majimbo yote ya Tanzania bara na visiwani.
“Hilo ndilo lengo letu kubwa kuwa na mgombea urais, tutasimamisha pia wagombea katika majimbo yote bara na visiwani. Tunao wanachama hadi Zanzibar,” alisema Kiyabo alipoulizwa kama wana mpango wa kumsimamisha mgombea urais katika uchaguzi ujao.
Hatua hiyo ya CCJ inaonyesha wazi kuwa sasa mgombea wa chama hicho atapambana na Rais jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu ujao kama atapitishwa na chama chake kuwania urais katika ngwe ya pili.
Kiyabo alisema CCJ imeanzishwa kuziba pengo la upinzani ambao sasa unaonekana kulegalega baada ya vyama vilivyopo kupoteza mwelekeo.
“Hakuna vyama vya upinzani vyenye nguvu nchini, wapinzani wamekalia kumsifia Rais Kikwete. Sisi tunadhamiria kuonyesha sera mpya zitakazoleta changamoto. Tunataka Watanzania wafurahie matunda ya rasilimali za nchi yao na pia wawe na uhuru wa kujitafutia maendeleo,”alisema.
Kiyabo ambaye ana taaluma ya Sayansi ya Jamii alisita kuwataja wadhamini wa chama hicho akieleza kuwa ni mapema mno kufanya hivyo sasa, ingawa baadhi ya vigogo wakubwa ndani ya CCM hususan ambao hawaridhishwi na mwenendo ndani ya chama hicho wanadaiwa kuwa wapo nyuma yake.
“Ukifika wakati wake tutawatajia, ila kwa sasa tunasisitiza kwamba hiki ni chama kilichoanzishwa na wananchi wenyewe.”alisema.
Hata hivyo, Katibu wa uenezi na itikadi wa CCM, John Chiligati alinukuriwa juzi akisema kuwa chama chao hakihofii usajili wa CCJ, ambacho kinahusishwa na baadhi ya vigogo wa chama tawala na upinzani, wakiwemo wabunge.
Alisema CCM bado ni imara na haiwezi kutikiswa na kuanzishwa kwa CCJ kwa kuwa haina ubavu wa kuimega CCM.
Chiligati alisema CCM imepokea taarifa za kuanzishwa kwa CCJ kama ilivyopokea taarifa za usajili wa vyama vingine vya siasa kwa kuwa uanzishwaji wake uko katika utaratibu wa sheria.
Mwenyekiti CCJ alitamba kwamba hadi kufikia mwishoni mwa Februari mwaka huu, watakuwa wamekamilisha masharti ya msajili wa vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na kuwa na wanachama 200 katika mikoa minane bara na mikoa miwili visiwani.
“Tutahakikisha tunakamilisha masharti ya msajili wa vyama vya siasa kabla ya kwisha Februari. Tumejiandaa vya kutosha hadi sasa tuna wanachama 2000 hapa jijini Dar es Salaam na pia tunao wanachama wengi mikoani,”alisema.
Naye Katibu wa muda wa chama hicho, Renatus Muabhi alisema CCJ kimeanzishwa kuleta mapinduzi ya kisiasa na kiuchumi miongoni mwa jamii ya watanzania na sio kuigawa CCM.Picha na habari za Elias Msuya na Sadick Mtulya.
Comments