Thursday, January 28, 2010

Aliyedaiwa kufa na kuzikwa aibuka hai



MKAZI wa mjini Mafinga ambaye alidaiwa kufa na kuzikwa mwezi Oktoba mwaka jana, amerejea kwao akiwa hai na kusema “sikumbuki kama niliwahi kufa”.
Kijana huyo, Nickson Kabonge, 23, aliwasili nyumbani kwao juzi mchana akitokea msitu wa Kihanga ulio Mafinga ambako amedai alikuwa akifanya shughuli za kupakia mbao na magogo kwenye magari.
Wakati familia yake, na hasa baba ikiamini kuwa alishafariki na ilishiriki kumzika, kijana huyo aliiambia Mwananchi kuwa aliamua kurejea kwao baada ya kuota kila mara kuwa baba yake amefariki.
Kurejea kwa kijana huyo kulizua yaharuki kwa wakazi wa mjini hapa ambao walifurika nyumbani kwao kumshangaa, wakionekana kutoamini kuwa aliyerejea ni kijana waliyemzika na badala yake kumchukulia kuwa ni msukule.
Pamoja na kurejea kwao, baba wa kijana huyo, Boniface Kabonge alisema kuwa mwanaye Nickson alifariki dunia Oktoba 6 mwaka jana na kuzikwa kwenye makaburi ya Mufindi.
“Nilishtuka mwanangu alipobisha hodi na kuingia ndani wakati najua alishakufa na tulimzika, sijui imekuwaje hadi aliyekufa arejee nyumbani,” alisema
Alisema kabla ya kifo chake kijana huyo alikuwa akifanya kazi ya kupasua mbao kwenye msitu huo wa Kihanga, lakini alifariki baada ya kuangukiwa na gogo ambalo lilimjeruhi vibaya kichwani.
Alisema mwili wa kijana huyo ulipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi na
kuhifadhiwa katika chumba cha maiti hadi siku ya pili ulipopelekwa nyumbani
kwao kwa ajili ya kuagwa.
“Mimi ndiye niliyemuosha mwanangu kutokana na mila zetu, tulimpeleka nyumbani watu waliaga kama kawaida na baadaye tulimzika kwa sababu kila mmoja alijiridhisha na kifo chake,” alisema
Akizungumza na Mwananchi kijana huyo alisema hafahamu habari za kifo chake.
“Nashangaa wanaponikimbia ila sikumbuki kama niliwahi kufa, nachojua nilikuwa nikiishi na wenzangu kumi katika msitu wa Kihanga ambako tulikuwa tukila pumba na maji,” alisema
Alisema kuwa kilichomrejesha nyumbani kwao ni ndoto alizokuwa akiota kuwa baba yake amefariki hali iliyomlazimu arudi kuhani msiba.
“Kila nikikaa mwili wa baba yangu ulikuwa ukipita mbele yangu kwenye jeneza huku ukiwa umefunikwa kitambaa chekundu, ndio maana nikaamua kuja kumzika. Nashangaa nilipofika hapa nikaambiwa kuwa mimi ndio nilikuwa nimekufa,” alisema. Tumaini Msowoya, Mufindi

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...