Thursday, January 14, 2010

Pinda atangaza mali zake


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ana kama Sh25 milioni kwenye akaunti yake, nyumba tatu za kawaida zilizo Dar, Mpanda na Dodoma na gari alilolinunua kwa mkopo.

Pinda, maarufu kama Mtoto wa Mkulima, aliweka bayana hayo wakati akitangaza mali zake kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika ofisini kwake.

"Na kikubwa ambacho mimi nasema kwa nafasi hizi (za uwaziri), pengine mimi sielewi unataka utajiri ili ufanye nini," alisema mbunge huyo wa Mpanda wakati akitangaza mali zake kutekeleza Sheria ya Maadili ya Uongozi.

Akijibu swali la mmoja wa wahariri, Pinda alisema kuwa ameamua kufanya hivyo kwa sababu ni utaratibu mzuri unaoweza kuweka wazi mali za viongozi ili wasije kupotoka kimaadili.

"Ninajitahidi kujaza fomu za sekretarieti ya maadili kila mwaka na ninazipeleka huko na kwa sababu sijaulizwa napenda niamini kwamba sijagombana na tume," alisema Pinda ambaye amekuwa naibu waziri wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na baadaye waziri kamili kabla ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu mapema mwaka juzi.

"(Waziri mkuu) Ana nyumba Dodoma kutokana na utaratibu wa mikopo ya nyumba za serikali; ana nyumba Mpanda ambayo imepatikana kwa mpango wa kawaida tu, imetokana na visenti kidogo akanunua pale ambapo bahati nzuri gharama za ujenzi si kubwa sana, akakikarabati kipo pale kipo Makanyagio pale."

"Haya! Ukitoka pale unataka niseme nini tena. Dar es Salaam sina nyumba ya kusema ya maana sana ukienda shambani Pugu kule kipo kinyumba kidogo hivyo inahitajika kazi ya ziada kuweza kufanya paonekane pa maana.

"Kijijini kwa baba yangu pale Kibaoni sina nyumba; pale mlipoona nimekaa na bibi tunapiga porojo, kile kijumba mimi na wadogo zangu tulimsaidia babu kwa ajili ya kumjengea babu yetu na pale ndipo nilipokuwa nafikia siku zote wakati wa likizo."

Pinda, ambaye amekuwa mbunge tangu mwaka 2000, alisema miaka yote alikuwa akifikia kwenye nyumba hiyo ambayo yeye ana chumba chake kimoja hali kadhalika babu yake. imeandikwa na Yahya Charahani.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...