Wednesday, January 27, 2010

Moto waunguza tena Bagamoyo





MOTO mkubwa umeteketeza, soko, vibanda vya kukaangia samaki na migawaha zaidi ya 40 katika eneo la bandarini mjini Bagamoyo.
Moto huo umewatonesha kidonda wakazi wa Bagamoyo ambao mwaka jana, walikumbwa na balaa la kuteketea kwa hoteli ya Paradise, moja ya miundombinu muhimu ya uchumi wa eneo hilo.
Jana majira ya saa 9:30 jioni moto mwingine mkubwa ulilipuka katika vibanda hivyo na hakukuwa na kikosi chochote cha Zimamoto kilichofika eneo hilo kuuzima hadi saa 10:00 gazeti hili lilipoondoka eneo la tukio.
"Hivi unavyoona vinaungua ni vibanda vya wakaanga samaki, pale kuna migahawa ya chai kwa ajili ya wavuvi wanaotia nanga wakitoka baharini," alifafanua mvuvi mmoja ambaye kwa wakati huo hakuwa tayari kutaja jina lake.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Magesa Mulongo, alipotafutwa kwa njia ya simu kutoa taarifa kamili ya hasara, simu yake hiyo ya kiganjani iliita bila majibu kama ilivyokuwa kwa Kamanda wa Polisi Mkoani humo Absolom Mwakiyomo, ambaye naye hakupokea simu.
Lakini, kwa mujibu wa Mvuvi huyo, moto huo ulipata msukumo mkubwa kutokana na upepo maarufu kama Kaskazi ambao mara nyingi huvuma kutoka Pwani kwenda Bara.
"Kwakweli wavuvi na wamiliki wa migahawa hii wamepata hasara kubwa kweli, hili ni eneo lao muhimu kiuchumi, kuungua kwa migawaha kutarudisha nyuma kasi ya shughuli za uchumi," alielezea tukio hilo ambalo gazeti hili imefanikiwa kupata picha za moja ya kibanda kilichokuwa kikiteketea.
Eneo hilo ni maarufu kwa wavuvi ambao hutia nanga kwa ajili ya kuuza samaki wao kwa wafanyabiashara mbalimbali ambao nao hukaanga na kuuza kwa wateja wengine mbalimbali.
Gazeti hili lililokuwepo eneo la tukio lilishuhudia moto huo ukitekeleza vibanda hivyo huku wamiliki wake wakijitahidi kuuzima bila mafanikio.
Uchunguzi wa awali wa Mwananchi, umebaini kwamba chanzo cha moto huo kilitoka ndani ya moja ya kibanda kati ya vilivyoungua eneo hilo la tukio. Imeandikwa na Christopher Buke.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...